Saturday, September 22, 2012

Waislam Dar es Salaam Waandamana Kulaani Filamu Iliyomkashifu Mtume


Baadhi ya waumini wa dhehebu la Kiislamu wakiandamana ikiwa ni hatua ya kulaani filamu iliyotengenezwa nchini Marekani ya kumkashfu Mtume (S.W.A)
Waumini wanawake wa dini ya Kiislamu wakiandamana jijini Dar es Salaam eneo la Kidongo Chekundu kulaani filamu ya kumkashfu Mtume wao iliyotengenezwa nchini Marekani

Mmoja wa waandamanaji akizungumza na vyombo vya habari kuelezea nia ya maandamano yao
Baadhi ya waumini wa dhehebu la Kiislamu wakiandamana ndani ya Uwanja wa Kidongo Chekundu Dar es Salaam  ikiwa ni hatua ya kulaani filamu iliyotengenezwa nchini Marekani ya kumkashfu Mtume (S.W.A).
Na Joachim Mushi
BAADHI ya waumini wa dini ya Kiislamu leo jijini Dar es Salaam wamefanya maandamano katika viwanja wa Kidongo Chekundu ikiwa ni hatua ya kuungana na Waislamu katika nchi mbalimbali kupinga filamu iliyotengenezwa nchini Marekani ikimkashfu kiongozi wao (Mtume) pamoja na dini ya Kiislamu.
Maandamano hayo yalianza majira ya mchana mara baada ya kumalizika kwa swala ya Ijumaa kwa misikiti mbalimbali hasa ile ya kati kati ya jiji, ambapo waumini waliongozana kuelekea katika Viwanja vya Kidongo Chekundi vilivyopo pembezoni mwa eneo la Mnazi Mmoja.
Taarifa za awali zilieleza awali waumini hao kupitia viongozi wao waliomba kibali cha kufanya maandamano kuelekea viwanja vya Jangwani lakini walizuiwa kutokana na uwanja huo kuwa na shughuli zingine. Baada ya kuzuiwa waliamua kuandamana kwenye eneo hilo bila kibali chochote lakini hakukuwa na kikwazo chochote.
Waandamanaji walionekana wameshika mabango yaliokuwa na ujumbe wa kuyalaani mataifa ya Marekani na Israel huku wakiitaka Serikali kufuta ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kutokana na filamu wanayoilalamikia kutengenezwa katika taifa hilo.

Vikosi vya FFU vikiwa tayari kupambana na waandamanaji endapo watavuka viwanja vya Kidongo Chekundu
Taarifa za awali zilidai kundi hilo la waandamanaji lilipanga kuelekea zilipo balozi za Marekani jambo ambalo halikufanyika zaidi ya kuishia kuzunguka katika viwanja vya Kidongo Chekundu chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kilichokuwa tayari kudhibiti vurugu zozote.
Magasi ya FFU pamoja na asikari wa kawaida walikuwa wamesheheni eneo moja la viwanja vya Kidongo Chekundu wakiwa na vifaa vyote vya kudhibiti/kukabiliana na aina yoyote ya vurugu na walikuwa wamezuia waandamanaji hao kuvuka eneo hilo.
Baadha ya kuzunguka kwa muda huku wakiimba nyimbo za kulaani kitendo kilichofanyika baadhi ya viongozi wa vikundi hivyo vya maandamano walipanda na kutoa matamko ya kulaani kitendo kilichofanywa dhidi ya Mtume, na kwa pamoja walitoa tamko la kuitaka Serikali kutoa tamko dhidi ya kitendo kilichofanyika ndani ya wiki moja na kinyume cha hapo watafanya maandamano makubwa kulaani zaidi.

Taarifa ya kuteuliwa Meja Jen. Samuel A. Ndomba kuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ


 
Picture
Meja Jen. Ndomba akila kiapo hivi karibuni (pica ya maktaba ya MoDewji blog)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Meja Jenerali Samuel Albert Ndomba kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Aidha, Rais Kikwete amempandisha cheo Meja Jenerali Ndomba kuwa Luteni Jenerali.

Taarifa iliyotolewa leo, Ijumaa, Septemba 21, 2012, mjini Dar Es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais – Ikulu, imesema kuwa uteuzi huo unaanza leo.

Taarifa hiyo ya Balozi Sefue imesema kuwa kabla ya uteuzi wake, Meja Jenerali Ndomba alikuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Jenerali Ndomba anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Luteni Jenerali Abdulrahman  A. Shimbo ambaye amestaafu Jeshi kwa mujibu wa sheria baada ya kufikisha umri wa miaka 60.

Taarifa ya Balozi Sefue pia imesema kuwa Rais Kikwete amemteua Brigedia Jenerali Raphael Mugoya Muhuga kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa kuanzia leo, Ijumaa, Septemba 21, 2012.

Aidha, Rais Kikwete amempandisha cheo Brigedia Jenerali Muhuga kuwa Meja Jenerali.

Kabla ya uteuzi wake, Brigedia Jenerali Muhuga alikuwa Mkuu wa Utawala na Mafunzo wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

21 Septemba, 2012

Tuesday, September 18, 2012

Majina ya Kata zitakazofanya uchaguzi mdogo wa Madiwani, Oktoba 2012

Tume ya Taifa ya Uchaguzi  (NEC), imetja majina ya Kata zitakazofanya uchaguzi mdogo wa Madiwani kutokana na wagombea walioshinda katika uchaguzi wa Madiwani uliofanyika Oktoba 31, 2010  baadhi yao kufariki, kupoteza sifa na kujiuzulu.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume hiyo, Jullius Mallaba, alisema maandalizi yamekamilika na upigaji kura utafanyika katika vituo vilivyotumika wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Aidha, Mallaba alisema watakaohusika katika upigaji kura ni wale walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura ambapo wapiga kura wanatakiwa kwenda kwenye vituo vya kupigia kura wakiwa na kadi zao.

Mallaba alizitaja kata hizo ambazo uchaguzi utafanyika ni:
  • Arusha - Bangata 
  • Arusha - Daraja Mbili
  • Dodoma - Msalato
  • Dodoma - Mpwapwa 
  • Pwani/Bagamoyo - Magomeni
  • Geita - Lwezera 
  • Shinyanga - Bugarama
  • Shinyanga - Mwananza
  • Tanga/Korogwe - Vugiri 
  • Tanga/Korogwe - Tamota 
  • Lindi/Liwale - Makata 
  • Lindi/Nachigwea - Mnero
  • Njombe/Ludewa - Mlangali
  • Njombe/Makete - Luwumbu
  • Ruvuma/Mbinga - Mpepai 
  • Ruvuma/Songea - Mletele
  • Tabora/Sikonge - Ipole
  • Tabora - Miyenze 
  • Tabora - Karitu
  • Mbeya/Mbozi - Mpapa
  • Mwanza/Misungwi - Lubili
  • Kilimanjaro - Kilema Kusini
  • Kilimanjaro - Nanjara
  • Kilimanjaro - Neha 
  • Morogoro/Mvomero - Mtibwa 
  • Morogoro/Ulanga - Mahenge
  • Mtwara/Nanyumbu - Likokona
  • Mtwara/Newala - Kitangiri