Tuesday, April 16, 2013

CAG Ataka William Mhando wa Tanesco na Mkewe Washitakiwe

 



Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh (kushoto) akiwa na Rais Kikwete.
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amemuweka kitanzini aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando, baada ya kushauri ashtakiwe pamoja na mkewe, Clara, kutokana ukiukwaji wa sheria katika kutoa zabuni.
Mbali na Mhando, wengine ambao CAG amependekeza wachukuliwe hatua za kisheria ni Mkurugenzi wa Kampuni ya McDonald Live Line Technology, watu wote walioingia katika biashara na Tanesco kinyume cha sheria pamoja na wafanyakazi waliohusika kutoa zabuni hizo.
Mapendekezo hayo ya CAG, Utouh yamo katika ripoti yake ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma ya 2011/12, aliyoiwasilisha bungeni wiki iliyopita ikirejea ukaguzi maalumu uliofanyika katika shirika hilo kutokana na maombi ya bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo. CAG pia ameweka wazi kuwa Tanesco iligubikwa na ukiukwaji uliokithiri wa Sheria ya Ununuzi ya 2004 na kanuni zake za mwaka 2005, uliosababishwa na viongozi wake wa juu.
“Mkurugenzi Mkuu wa Shirika akiwa ndiye mwenye uamuzi wa kuhusu ununuzi, alishindwa kuzuia ukiukwaji huu wa sheria ya ununuzi na mara nyingi aliidhinisha ununuzi wa chanzo kimoja au usiozidi ushindani,” inasema ripoti hiyo na kuongeza:
“Bodi inatakiwa kuripoti kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DPP) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) yale yote yaliyogunduliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kubaini kuwapo kwa rushwa na ubadhirifu.”
Katika ripoti hiyo, CAG amebainisha ukiukwaji mkubwa wa sheria uliofanywa na Mhando, huku akibainisha kuwa mkewe, ambaye ni Mtendaji wa Mkuu wa Kampuni za Santa Clara Supplies Company Limited, alipewa zabuni katika shirika hilo kwa kutumia taarifa za kughushi. Pia CAG amebainisha kuwa kampuni hiyo haikuwasilisha katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), rejesho la kodi kiasi cha Sh4.854 milioni ilizolipwa na Tanesco.
Santa Clara
CAG amebainisha kuwa kampuni hiyo iliyosajiliwa Aprili 18, 2011, ilipewa Leseni ya Biashara, Mei 2011 na kwamba wakurugenzi na wanahisa wa kampuni ni mke na watoto wawili wa Mhando. Mke wa Mhando aliwahi kuwa mfanyakazi wa Tanesco, lakini aliacha kazi baada ya mumewe kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu.
CAG amebainisha kampuni hiyo iliingia mkataba na Tanesco na kupewa zabuni Namba PA/001/11/HQ/G/011 ya ugavi wa vifaa vya ofisi, vifaa vya matumizi ya kompyuta na mashine za kudurusu, kwa mwaka 2011 hadi 2012, mkataba ulianza Desemba 20, 2011.

Rais Kikwete Aomboleza Kifo cha Meja Jenerali Makame

Jeneza lenye mwili wa marehemu Meja Generali Makame Rashid ukiwasili kwenye viwanja vya Makao Makuu ya JKT jijini Dar es Salaam kwa ajili ya shughuli ya kuaga,marehemu Meja Generali Makame Rashid, aliyefariki dunia jana katika Hospitali ya TMJ, jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais Dk. Bilal, akitoa salamu za mwisho kwa mwili wa Meja Generali Makame Rashid.
Makamu wa Rais Dk. Bilal, Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na Mkuu wa Majeshi Davis Mwamunyange wakiwa katika hafla ya kuaga mwili wa Meja Generali Makame Rashid.
Mkuu wa jeshi la polisi Nchini IGP Saidi Mwema (Katikati)akiwa na Luteni Jenerali S.A. Ndomba Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (Kushoto) na Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP), John Minja (Kulia). Picha zote na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Mstaafu Makame Rashidi, ambaye ameaga dunia alfajiri ya Aprili 14, 2013 katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo, Dar Es Salaam.
Enzi za uhai wake, mbali na kuwa mkuu wa JKT, Meja Jenerali Makame pia alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Balozi wa Tanzania katika Malawi. Kufuatia msiba huo, Rais Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange kuomboleza kifo hicho.
Rais Kikwete ameeleza kuwa alimfahamu Jenerali Makame enzi za uhai wake kwa miaka mingi katika utumishi wa umma. Alimfahamu kama mtumishi mtiifu na msikivu ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kama kiongozi mwadilifu na mwaminifu katika nafasi yake ya Ukuu wa Mkoa na kama Mwanadiplomasia mahiri ambaye aliiwakilisha Tanzania nje ya nchi kwa uhodari mkubwa.
Katika salamu hizo, Rais Kikwete amemwambia Jenerali Mwamunyange: “Nimepokea kwa masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Meja Jenerali Mstaafu Makame Rashid ambaye nimejulishwa kuwa ameaga dunia asubuhi ya leo kwenye Hospitali ya Lugalo. Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo hiki.”
Ameongeza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Nakuomba kupitia kwako vile vile unifikishie salamu zangu za rambirambi kwa maofisa wote wa Jeshi letu ambao wameondokewa na ofisa mwenzao na askari wote ambao wameondokewa na kiongozi wao. Aidha, kupitia kwako, naitumia familia ya Marehemu Makame Rashid pole nyingi kwa msiba huu mkubwa wa kuondokewa na mhimili wa familia.”
“Nakuomba uwajulishe kuwa niko nao katika msiba huo mkubwa kwa sababu naelewa huzuni na machungu yao katika kipindi hiki kigumu. Nawaombea subira za Mwenyezi Mungu awavushe katika kipindi hiki. Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenye Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Makame Rashid. Amina”
Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete asubuhi ya Aprili 14, 2013 amekwenda kuwajulia hali wafiwa nyumbani kwa Meja Jenerali Mstaafu Makame Rashid eneo la Mikocheni, mjini Dar Es salaam.