MAELEZO NA HOJA BINAFSI YA KUPENDEKEZA BUNGE LIJADILI NA KUPITISHA
MAAZIMIO YA HATUA ZA HARAKA ZA KUBORESHA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA
USHUGHULIKIAJI WA MAJI TAKA KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM KWA MUJIBU WA KANUNI YA
54 FASILI YA (1) YA KANUNI ZA KUDUMU ZA BUNGE TOLEO LA MWAKA 2007
Mheshimiwa Spika;
Awali
ya yote niungane na wote wenye mapenzi mapema katika kuomba ulinzi wa Mwenyezi
Mungu wakati tukitimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba
ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania wa kuwawakilisha wananchi, kuisimamia
serikali, kuidhinisha mipango na kutunga sheria.
Mheshimiwa Spika;
Aidha,
kwa namna ya pekee ni kushukuru wewe binafsi na uongozi mzima wa Bunge kwa
kunipa fursa hii adimu na adhimu ya kuwasilisha hoja binafsi kwa mujibu wa kanuni
ya 54 fasili ya (1) ya kupendekeza bunge lijadili na kupitisha maazimio ya
hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji
wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.
Mheshimiwa Spika;
Maji
ni uhai, hivyo matatizo ya upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji
taka katika Jiji la Dar es salaam na nchini kwa ujumla kama hatua za haraka
zisipochukuliwa yatageuka kuwa janga la taifa. Katika kila watanzania katika
Jiji la Dar es Salaam na nchini; kwa wastani mmoja hapati huduma ya maji safi
na salama na hali ni mbaya zaidi kuhusu ushughulikiaji wa maji taka.
Wakati
baadhi ya nchi duniani zikielezwa kwenye kitabu cha hivi karibuni cha Mnukuzi
Maalum wa Umoja wa Mataifa (UN Special Rapporteur) kuwa katika mwelekeo
unaostahili kuhusu kuhakikisha haki ya maji na usafi wa mazingira (On the right
track; Good practices in realizing the rights to water and sanitation: 2012),
hali ni kinyume kwa taifa letu.
Ripoti
ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya maji (WaterAid: 2011)
imeiweka Tanzania katika kundi la nchi ambazo haziko katika mwelekeo
unaostahili wa kuboresha upatikanaji wa maji safi, ushughulikiaji wa maji taka
na usafi wa mazingira (Policy Report: Off Track, Off Target; why investments in
water, sanitation and hygiene is not reaching those who need the most).
Mheshimiwa Spika;
Hoja
hii inalengo la kuibua mjadala wa hatua za haraka. Kimsingi hatua hizi za
haraka hazitanufaisha Mkoa mmoja pekee kwa kuzingatia kuwa Mpango Maalum wa
kutatua tatizo la maji katika Jiji la Dar es salaam ni kwa ajili pia ya maeneo
mengine ya miradi iliyo sehemu ya mpango huo ya Morogoro mpaka Pwani. Aidha,
kujadiliwa na kupitishwa kwa mapendekezo ya hoja hii kutaongeza pia msukumo wa
miradi katika maeneo mengine ya mijini na vijijini katika mikoa mbalimbali
nchini.
Shukrani
zangu za dhati ziwafikie wabunge wenzangu wa vyama vya upinzani na wa chama
tawala kwa maoni na mapendekezo yenu yaliyoniwezesha kuirekebisha hoja hii
pamoja na ushauri wa Katibu wa Bunge Dr Thomas Kashillilah na maafisa na watendaji katika ofisi ya bunge,
kambi rasmi ya upinzani na ofisi ya mbunge wa Jimbo la Ubungo mlioboresha hoja
hii kwa manufaa ya Jiji la Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika;
Nitumie
pia nafasi hii kuwashukuru Watanzania wenzangu wa kada, hadhi na ngazi
mbalimbali katika taasisi na maeneo mengi ndani na nje ya nchi mnaoendelea
kuniunga mkono kwa hali na mali katika kutimiza majukumu yangu ya kibunge na
nafasi nyingine ninazozitumikia.
Nawashukuru
sala zenu wakati wa kesi ya msingi na rufaa ya kupingwa kwa matokeo ya ushindi
wetu Jimbo la Uchaguzi la Ubungo; kwa pamoja tumeshinda, tuendelee na kazi.
Aidha,
pamoja na mjadala huu wa bungeni natarajia kupokea maoni na mapendekezo yenu
kuhusu hoja hii kwa njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo kupitia mtandao wa http://mnyika.blogspot.com
kwa hatua zaidi. Kaulimbiu yetu ni ile ile: AMUA; Maslahi ya Umma Kwanza.
MAELEZO YA HOJA:
Mheshimiwa Spika;
Maji ni mojawapo ya mahitaji ya msingi ya binadamu, maji ni
uhai. Upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ni sehemu ya muhimu ya
maendeleo ya nchi na maisha ya wananchi. Maji ni lazima kwa matumizi ya
majumbani, maji ni muhimu ni moja ya malighafi muhimu katika kazi za uzalishaji
iwe ni za viwanda, kilimo, mifugo na shughuli zingine za kiuchumi.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni nchi ambayo
imejaliwa vyanzo vingi vya maji, vinavyohusisha mito, mvua, maziwa na bahari;
kuwepo kwa vyanzo hivi vya maji ni wazi kuwa nchi yetu inaweza kuepukana na
shida ya maji inayoikumba jamii ya Tanzania iwapo tutaondoa udhaifu uliopo.
Aidha, udhaifu huo unahusisha pia kuziweka vyanzo vyenyewe pia mashakani kwa
matendo ya binadamu yenye kuathiri endelevu wa matumizi hali itayozua migogoro
katika siku za usoni iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Mheshimiwa Spika;
Upatikanaji wa maji safi na salama kwa urahisi wa bei
unachangia katika kupunguza gharama za maisha; upatikanaji wa maji safi na
salama karibu na makazi husaidia jamii, hususan wanawake, kutumia nguvu na muda
katika uzalishaji na hivyo kuchangia katika kupunguza umaskini. Upatikanaji wa
maji safi na salama ni nyenzo ya kulinda utu na afya; kinyume chake kuenea kwa
magonjwa na maisha duni.
Ifahamike kuwa kadiri
ya Tathmini ya Hali ya watu na Afya ya mwaka 2010 (Demographic and Health
Survey 2010); ni asilimia 4.8 tu ya kaya zilizopo vijijini ndiyo zinazopata
maji katika eneo lao la kaya (water on
premises) wakati ni asilimia 19.4 tu ya kaya kwa mijini ndizo zenye maji
katika kaya zao. Hivyo kaya nyingi za
Tanzania zinawekwa katika mazingira hatarishi kwa magonjwa ya mlipuko na
mengine ambayo si ya mlipuko kutokana na uhaba wa maji, hali ikiwa tete zaidi
katika maeneo yasiyopimwa yenye msongamano mkubwa wa watu katika Jiji la Dar es
Salaam (slums).
Mheshimiwa Spika;
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977,
toleo la mwaka 2005 haijataja haki ya kupata maji safi na salama; huu ni kati
ya upungufu ambao wananchi wa mijini na vijijini wanapaswa kuutolea maoni
katika mchakato wa katiba mpya kwa kurejea mfano wa Katiba ya Afrika Kusini,
Ghana na katiba mpya ya Kenya.
Katika hatua ya sasa haki hii inapaswa kulindwa kupitia
Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni (“The
International Covenant on Economic, Social and Cultural Rights”,
ICESCR) wa 1966. Mkataba huu unataja
haki za kijamii na hivi karibuni Umoja wa Mataifa (UN) umeutafsiri kuwa ni
pamoja na haki ya kupata maji safi na salama ambayo inapaswa kutiliwa mkazo
katika nchi yetu.
Suala
la upatikanaji wa maji safi na kuweza kushughulia maji taka ni sehemu ya
makubaliano ya kimataifa ambayo nchi yetu imeridhia kuingia mathalani Malengo ya Milenia (MDGs); lengo
namba saba (7) shabaha 10; la kupunguza nusu ya watu waoishi bila maji na safi
ya kunywa na usafi wa msingi. Hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji
safi na ushughulikiaji wa maji taka ni muhimu kama sehemu ya haki za binadamu
lakini lina tija pia katika uzalishaji na uchumi wa nchi kwa kuwa tafiti
zinaonyesha kwamba kudumu kwa matatizo hayo kunazigharimu nchi za Afrika,
Tanzania ikiwemo wastani wa asilimia sita (6) ya pato la taifa (Gross Domestic Product).
Utafiti
uliofanywa kwa Stockholm Environment Institute kwa kushirikiana na Benki ya
Maendeleo Afrika mwaka 2006 kuhusu uhusiano kati ya maji na umaskini Afrika kwa
kutumia mfano wa nchi yetu (Water and Poverty Linkages in Africa: Tanzania Case
Study) umebainisha namna ilivyo vigumu kupima Tanzania inavyosonga mbele katika
utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia yanayohusu maji. Aidha, utafiti
huo umeeleza namna ambavyo bila kushughulikia kwa haraka matatizo ya maji
jitihada za kupambana na umaskini zitakwama.
Mheshimiwa Spika;
Jiji
la Dar es Salaam ni letu sote, ni mahali ambapo wabunge wote tunaishi kwa
nyakati mbalimbali hususan wakati wa vikao vya kamati za kudumu za Bunge hivyo
adha ya maji katika Jiji hili kila mmoja anaifahamu na anawajibu wa kushiriki
katika kuipatia ufumbuzi.
Kwa
mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2002 Mkoa wa Dar es salaam ulikuwa na
jumla ya wakazi 2,497,940 huku ukikadiriwa kuwa na kasi ya ongezeko la watu ya
asilimia 6 kwa mwaka; ikiwa ni juu ya wastani wa kitaifa wa asilimia 4.5,
lakini kasi ya upatikanaji wa maji na ushughulikiaji wa maji taka ikiwa ndogo. Bunge ikiwa ni chombo cha juu cha kuisimamia Serikali
linapaswa kuitafakari hali hii kwa upekee wake kwa kuwa itakuwa na athari kwa
taifa kwa sasa na baadaye ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.
Hadi
kufikia mwaka 2011 Jiji la Dar es Salaam linakadiriwa kuwa na watu zaidi
milioni nne na laki tano likiwa na takribani nusu ya waajiriwa wote wa
viwandani nchini. Hivyo kwa kurejea takwimu za ujumla za sensa zilizotolewa
mwezi Desemba 2012 kwamba Tanzania kwa sasa ina watu zaidi ya milioni 44.9;
hoja hii inalenga kupendekeza kwa bunge kujadili kuhusu mustakabali wa zaidi ya
asilimia 10 ya Watanzania, lakini kwa kurejea utangulizi wangu maazimio
ninayopendekeza yapitishwe yatakuwa na maslahi sio kwa wakazi wa Dar es salaam
bali kwa taifa kwa ujumla mijini na vijijini.
Mheshimiwa Spika;
Upatikanaji
wa maji katika Jiji la Dar es salaam miaka michache baada mwaka 1961 ulikuwa
zaidi ya asilimia 68; hivi sasa miaka 50 baada ya uhuru tumerudi nyuma na
upatikanaji ni kwa wastani asilimia 55 tu tena kwa mgawo.
Zipo
hisia kwamba Dar es salaam inapata huduma maji safi na maji taka kuliko miji na
mijiji mengine nchini, lakini uhalisia unaonyesha kwamba hali ni bora kwa
wachache wakati walio wengi hususan waoishi kwenye maeneo ya wananchi wa kipato
chini hali ya upatikanaji wa maji ni duni kuliko miji na majiji mengine nchini.
Jiji
la Dar es Salaam ni la mwisho kwa kigezo cha wastani wa kitaifa wa upatikanaji
wa maji ukilinganisha na majiji mengine ambayo yanafikia asilimia 75; hivyo
hatua za haraka zinahitajika kurekebisha hali hiyo.
Hatua
hizo zitawezesha kupunguza kwa haraka tatizo hilo na kuelekeza nguvu zote
katika maeneo ya vijijini palipo na shida kubwa badala ya mfumo wa sasa ambapo
kwa miaka zaidi ya kumi, rasilimali zinatumika lakini kunakosekana ufumbuzi
endelevu maeneo yote.
Hatua
za haraka zinapaswa kuchukuliwa kuhusu hali hii kwa kuzingatia kuwa idadi ya
watu katika Jiji la Dar es salaam inaendelea kukua kwa kasi likiwa ni jiji la
tatu kwa ongezeko kubwa la watu barani Afrika na la tisa duniani; matatizo ya
upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika jiji kutokana na
msongamano wake wa watu ni bomu la wakati.
Mheshimiwa Spika;
Mkoa wa Dar es Salam unapata maji
kutoka mito na visima kwa matumizi ya nyumbani, viwanda, bustani, mifugo, usafi
na Mazingira. Sehemu ya Jiji inayopata maji inahudumiwa na Kampuni ya DAWASCO
(Dar es salaam Water Supply and Sewerage Company) ambayo imepewa mkataba na
Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam, DAWASA (Dar es Salaam Water
Supply and Sewerage Authority) na maeneo yasiyo na mtandao wa DAWASA hupata
maji kutoka visima vinavyoendeshwa na vyombo vya watumia maji, Taasisi na watu
binafsi.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Jimbo la Ubungo kama sehemu ya Jiji la Dar es
salaam katika kufuatilia masuala ya maji nilianza kwa kufanya Kongamano la Maji
mwanzoni mwa mwaka 2011 ili kuwakutanisha wananchi, mamlaka husika na wadau
wengine katika kuunganisha nguvu kupata ufumbuzi. Nikiri kwamba katika hatua za
awali ushirikiano kutoka DAWASA, DAWASCO na Wizara ya Maji ulikuwa mdogo kwa
kiwango cha kuamua kuwaunganisha wananchi kupitia ‘maandamano ya maji’ kwenda
DAWASCO. Toka wakati huo ushirikiano umeongezeka kwa upande wa DAWASCO ambapo
nimeshafanya nao ziara ya kikazi ya kata mbalimbali ya kutembelea maeneo yenye
matatizo na hatua zimechukuliwa ambazo zimewezesha baadhi ya maeneo kuanza
kutoka maji. Wakati wa hatua hizo tumewaonyesha DAWASCO biashara haramu ya maji
iliyokuwa ikiendelea na baadhi ya maeneo wamechukua hatua ikiwemo kwa watendaji
wao; hatua zaidi zinahitajika.
Mheshimiwa
Spika;
Baada ya mwito wa mara kadhaa hapa bungeni; nashukuru pia
Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe alifika Jimboni Oktoba 2012 kwa ajili ya
uzinduzi wa visima katika maeneo ya King’ongo, Kilungule na Mavurunza na kuona
hali halisi ya ugumu wa upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Dar es salaam.
Natambua pia jitihada zinazofanywa na wadau wengine wa
maendeleo Jimboni Ubungo katika masuala ya maji hususani Shirika la Kibelgiji
(BTC) katika maeneo ya Kwembe na Kibamba. Hata hivyo, yapo bado maeneo mengi
yenye matatizo makubwa ya maji ikiwemo ya Msumi, Makabe, Msakuzi,
Malambamawili, Msingwa, Goba na mengineyo mengi katika Jiji la Dar es salaam.
Na hata yale yenye miundombinu ya maji kama Sinza, Manzese, Makurumla na
mengine nayo hali ni tete. Hali iko hivyo katika Manispaa zote tatu za Ilala,
Kinondoni na Temeke.
Mheshimiwa Spika;
Hata
katika maeneo ya umma ya kuuzia maji, bei ipo juu kwa kuwa mamlaka zetu za
kuratibu na kusimamia masuala ya bei kama EWURA imekuwa na udhaifu katika
kusimamia na kuratibu bei elekezi wanazozitoa. Kwa mfano jiji la Dar es Salaam:
vituo vingi vya kutoa huduma za maji chini ya DAWASCO/DAWASA maarufu kama
“vioski vya maji” vimekuwa vikiongeza bei tofauti na bei elekezi toka EWURA ya
Tsh 1 kwa lita moja yaani ndoo ya lita 20 kwa Sh 20 kinyume na waraka nambari
10-017 (Order No.10.017) wa Juni 8, 2010, agizo lililopaswa kuanza kutekelezwa
Juni 15, 2010.
Utafiti
wa Shirika lisilo la kiserikali la Twaweza uliofanywa katika maeneo mbalimbali
ya jiji la Dar es Salaam uliopewa jina; “Bei
ya maji Dar es Salaam Je, wanaoendesha maghati ya maji wanazingatia bei
walizopangiwa?” uliweza kubainisha kukithiri kwa bei zilizoongezwa kinyume
na taratibu na agizo hilo la EWURA katika maghati ya maji. Hata baada ya
kurekebishwa kwa agizo hilo na bei kuongezwa kiasi bado maeneo hayo ya kuuzia
maji kwa umma yamekuwa yakipandisha bei kupindukia.
Mheshimiwa Spika;
Kero
kubwa zaidi iko wa wauzaji binafsi ambapo mazingira ya upungufu na ukubwa wa
mahitaji umefanya maji yauzwe kama bidhaa ya anasa bila mamlaka EWURA kutunga
kanuni wala kudhibiti bei, na kuachia soko holela yenye kuambana na hujuma za
miundombinu katika baadhi ya maeneo ili kuongeza uhaba.
Wananchi
ambao wengi wao ni wa kipato cha chini hupata huduma ya maji kwa gharama kubwa
ambayo huuzwa kwa kati ya Tsh 300 hadi Tsh 500 kwa ndoo ya lita 20 kwa maeneo
ya Dar es salaam.
Kuwapo
pia kwa watoa huduma wasio rasmi husababisha bei ya maji kuwa kubwa ambapo
inakadiriwa kuwa 68% ya wakazi wanaoishi maeneo ya mjini yenye msongamano
mkubwa hupata maji kutoka kwa wauzaji wasio rasmi.
Hatua
za haraka zinahitajika kudhibiti ongezeko kubwa la bei ya maji kwa wananchi wa
kipato cha chini wanaotegemea kupata maji kutoka sekta binafsi ambapo
wanaonunua maji kwa madumu hununua bei ambayo ni takribani mara 15 ya bei ya
mteja anayepata huduma ya maji ya bomba.
Mheshimiwa Spika;
Kwa
nyakati mbalimbali katika kipindi cha kati ya mwaka 2000 mpaka 2012 Serikali
imekuwa ikitoa ahadi bungeni ya kumaliza tatizo la majisafi na majitaka katika
Jiji la Dar es Salaam bila utekelezaji sahihi, kamili na wa haraka.
Malengo
ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini wa kwanza (MKUKUTA I)
yaliyoingizwa pia katika ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2005-2010 hayakuweza
kutekelezwa.
Malengo
mengine yameingizwa katika ilani ya CCM na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa
Umaskini awamu ya pili (MKUKUTA II) ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na
usafi wa mazingira ifikapo mwaka 2015; nayo tukiwa mwaka 2013 mwelekeo
unaonyesha kwamba hayatafikiwa iwapo hatua za haraka zisipochukuliwa.
Mara
baada ya kupitishwa kwa Mpango Maalum wa Maji katika Jiji la Dar es salaam
mwaka 2011, Rais alitangaza kwamba tatizo la maji kuwa historia mwaka 2013;
ambapo ni mwaka huu. Hata hivyo, utekelezaji wa mipango hauashirii ahadi hiyo
kutekelezeka na kwa mwelekeo wa sasa tatizo litaendelea mpaka baada ya mwaka
2016 iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Mheshimiwa Spika;
Mabomba ya ‘mchina’ bila maji na
miradi hewa katika maeneo ya wananchi wa kipato cha chini Jijini Dar es Salaam:
Kati
ya mwaka 2003 mpaka 2010 Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa
miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo
na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP).
Mradi
huo uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi
mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji huku kukiwa na
upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati wa usafirishaji, udhaifu katika
usambazaji na tuhuma za ufisadi katika matumizi.
Hali
hii ni kati ya matatizo yanayokera wananchi wa Jiji la Dar es salaam kwa kuwa
na mabomba yasiyotoa maji kwa muda mrefu hata kwa mgawo maarufu mitaani kama
mabomba ya ‘mchina’.
Serikali
ilieleze bunge lako sababu ya mabomba hayo kutokutoa maji mpaka hivi sasa, lini
mabomba hayo yataanza kutoa maji katika maeneo ambayo maji hayatoki mpaka sasa
na hatua gani zimechukuliwa wa waliotekeleza mradi huo bila kuzingatia
maandalizi ya msingi.
Ni
muhimu hatua zikachukuliwa kwa wahusika kwa kuwa kitendo cha mabomba hayo kukaa
muda mrefu bila kutoa maji inafanya miundombinu hiyo kuanza kuharibika au
kuharibiwa ambayo ni hasara kwa taifa kwa kuwa pamoja na fedha zilizotumika
kuweka mabomba hayo kupotea, fedha nyingine zitatumika katika hatua ya baadaye
kufanya matengenezo kwenye maeneo yaliyoharibika.
Aidha,
yapo pia malalamiko ya kwamba yapo maeneo ambayo yalitoa maji mara chache kati
ya mwaka 2009 na 2010 lakini baada ya hapo maeneo hayo hayajatoa maji tena
mpaka sasa, Serikali itoe maelezo ya kitaalamu kwa bunge na kwa wananchi kuhusu
sababu za maji hayo kutoka wakati huo na kutokutoka tena na hatua
zinazochukuliwa kurekebisha hali hiyo.
Mheshimiwa Spika;
Kasoro
katika mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka
Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water
Supply and Sanitation Project-DWSSP); hazielezwi na wananchi pekee bali pia
hata watafiti mbalimbali.
Ripoti
ya karibuni kabisa mwaka 2012 ya Shirika la Kimataifa la Water Aid ya utafiti
uliofanywa ukihusisha wataalamu kutoka Overseas Development Institute na Chuo
kimoja cha nchini Uingereza (SOAS) iliyofuatilia uwekezaji wa miradi ya maji
mijini katika nchi za Ghana, Burkinafasso na Tanzania ( Stregthening pro poor
targeting of investments by African utilities in urban water and Sanitation)
ikiwemo namna miradi ilivyoshindwa kuwajali maskini na maeneo na kiwango cha
hali ya maji kutokupatikana kinyume na malengo yaliyowekwa wakati wa kuanza kwa
mradi.
Mheshimiwa Spika;
Matatizo
ya kuwa na mabomba yasiyotoa maji hayapo tu katika mabomba waliyofungiwa
wananchi majumbani bali pia kwenye visima na ‘vioski’/maghati ya jumuiya. Kuna
udhaifu wa kuanzisha miradi ya jamii na kuacha kusimamia uendelevu
(sustainability) wake na hatimaye baada ya muda mfupi miradi hiyo iliyotumia
fedha za umma inabaki kuwa ‘miradi hewa’.
Utafiti wa vituo vya maji uliofanywa June 2009 na Overseas
Development Institute (ODI) chini ya udhamini wa shirika la Water Aid hapa
nchini ulibainisha ni asilimia 54 tu ya vituo vya maji vilivyopo ndivyo
vinatumika kwa kutoa huduma ya maji.
Hivyo kwa wastani baada ya miaka miwili tu ya kujengwa karibu nusu
ya visima na vioski huwa haviendelei tena kufanya kazi. Utaratibu wa kukimbilia kutumia fedha za
miradi ya maji kwa mwaka wa kibajeti mpya bila kuzingatia taarifa za
utekelezaji na ufuatiliaji wa miradi ya nyuma ni hatari kwa uendelevu wa kuwepo
kwa huduma ya maji kwa siku zijazo kama hatua za haraka hazitachukuliwa
kuzingatia matatizo yaliyojitokeza katika miradi iliyopita na kuzingatia ubora
na ufanisi katika miradi ya maji nchini.
Mheshimiwa Spika;
Utafiti uliofanywa na Economic and Social Research Foundation,
umebaini utofauti wa utekelezaji wa miradi ya serikali na mashirika binafsi
katika kauhakiki ubora wa matumizi ya fedha na huduma kwa jamii. Utafiti
ulibaini kuwa katika miradi iliyofadhiliwa na mashirika ya maendeleo, wastani
wa asilimia 67 ya vioski vilionekana kufanya kazi; wakati miradi ambayo
imefadhiliwa na Serikali ni wastani wa asilimia 45 ya vioski vya maji vilikuwa
vikifanya kazi katika maeneo hayo hayo. Utafiti huo ulihusu Mikoa ya Singida na
Dodoma.
Hali ni mbaya zaidi kwa upande wa Dar es Salaam ambapo kwa mujibu
wa utafiti mwingine wa Shirika la Water Aid uliobainisha kuwa asilimia 85 ya
vioski vilivyounganishwa Jijini Dar es Salaam havitoi maji, Asilimia 10 vinatoa
maji kwa kusuasua na asilimia 5 tu ndivyo ambavyo vinatoa maji kwa uhakika.
Mheshimiwa Spika;
Kasoro katika utendaji na
uwajibikaji wa mamlaka na vyombo vinavyohusika na utoaji na udhibiti wa huduma
ya maji:
Majukumu
ya utoaji wa huduma ya maji jijini Dar es salaam na baadhi ya maeneo ya Kibaha
na Bagamoyo yanafanywa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) ambayo ni
mmiliki, mkodishaji na msimamizi wa utoaji wa huduma ya majisafi na maji taka
na ina wajibu wa kupanga na kugharamia utekelezaji wa miradi ya miundombinu,
kuiendeleza na kugharamia matengenezo ya dharura na makubwa.
Mwaka
2005 DAWASA iliingia mkataba wa miaka kumi (10) wa uendeshaji na Shirika la
Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO). Chini ya mkataba huo majumu ya
DAWASCO ni kuendesha mitambo, kusimamia usambazaji wa maji na uondoshaji wa
maji taka, kuuza maji kwa wateja , kutoa ankara kwa wateja, kukusanya maduhuli,
kulipia gharama za uendeshaji, kutekeleza matengenezo makubwa yanayogharamiwa
na DAWASA na kutekeleza uunganishaji wa maji kwa wateja wapya kwa kutumia mfuko
wa maji.
Kisheria
na kimkataba DAWASA ina wajibu wa kuisimamia DAWASCO iliyoingia nayo mkataba;
hata hivyo kwa kuwa yote ni taasisi na mashirika ya umma ambayo bodi zake na
watendaji wake wakuu huteuliwa na mamlaka zile zile na kuripoti kwa watu wale
wale, hali ambayo ina athari kwenye utendaji na uwajibikaji.
Wakati
umefika sasa wa mkataba huo kati ya DAWASA na DAWASCO kuwekwa wazi kwa umma;
kufanyiwa tathmini ya miaka zaidi ya mitano iliyopita ya utekelezaji; kufanyiwa
marekebisho kwa ajili ya kipindi kilichobaki na maandalizi kuanza ya mfumo bora
unaopaswa kuanza kuandaliwa baada ya kuisha kwa mkataba huo mwaka 2015.
Utoaji
wa huduma ya maji unamhusu pia mdhibiti ambaye ni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma
ya Nishati na Maji (EWURA) yenye mamlaka ya kudhibiti utoaji wa huduma,
kuidhinisha bei ya huduma ya maji safi na uondoaji wa maji taka pamoja na kutoa
leseni za uendeshaji. Hata hivyo, EWURA imekuwa ikitoa kipaumbele zaidi kwenye
kutumia mamlaka yake kudhibiti kwa karibu sekta ya nishati, huku udhibiti kwenye
sekta muhimu ya maji hususan kwa upande wa watoa huduma binafsi ukiachwa uwe
katika mfumo wa soko holela na kuchangia katika ongezeko la bei ya maji pamoja
na ubovu wa huduma.
Wakati umefika sasa wa
Bunge kusimamia kwa karibu utekelezwaji wa
The Energy and Water Utilities Regulatory Authority Act (Sura ya 414)
kifungu cha 6 ambayo inaelekeza bayana kwamba wajibu wa EWURA ni pamoja na
kulinda maslahi ya walaji na kuhamasisha upatikanaji wa huduma inazozidhibiti
ikiwemo maji wa watumiaji wakiwemo wa kipato cha chini na walio pembezoni au
katika mazingira magumu (low income and disadvantaged consumers).
Aidha kwa mujibu wa
kifungu cha 7 cha sheria hiyo majukumu ya EWURA ni pamoja na kupanga viwango
cha ubora, viwango vya ugavi, kufuatilia utendaji ikiwemo uwekezaji na
upatikanaji, kudhibiti bei na tozo na kushughulikia malalamiko na migogoro.
EWURA itumie mamlaka
yake pia kwa kutumia vifungu vya 16, 17, 18 na 19 kuhakikisha kwamba masuala ya udhibiti wa bei
hashaishii tu katika mamlaka za umma na pia ianze yenye uchunguzi juu ya
kuporomoka kwa kiasi na kiwango cha huduma za maji katika Jiji la Dar es salaam
na nchi kwa ujumla na kupendekeza hatua za ziada za haraka zaidi kuweza
kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika;
Mwaka
2011 Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alifanya ukaguzi wa ufanisi
(performance audit) kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya
mijini ikiwemo Dar es salaam, hata hivyo taarifa yake ya Januari 2012 baada ya
kutajwa bungeni miongoni mwa hati zilizowasilishwa; hatua za kutekeleza
mapendekezo yake hazikupata usimamizi wa kutosha wa kibunge.
Hivyo,
ipo haja kwa kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa niaba ya Bunge
ipokee maelezo ya Serikali kuhusu utekelezaji wa mapendekezo yaliyomo kwenye
ripoti hiyo ambayo yalilenga kuboresha utendaji wa DAWASA, DAWASCO na Mamlaka
zingine za maji katika mikoa yote nchini na hatimaye kamati hiyo iwasilishe
maoni na mapendekezo yake bungeni kwa ajili ya hatua zaidi.
Mfumo duni wa ushughulikiaji wa
maji taka ni bomu la wakati katika Jiji la Dar es salaam:
Mheshimiwa Spika;
Hali
ni mbaya zaidi kuhusu uondoaji wa maji taka ambapo ni chini ya asilimia 10 tu
ya makazi ndiyo yaliyounganishwa katika mtandao wa maji taka na hivyo kuleta
uchafuzi wa mazingira hususani katika maeneo yasiyopimwa. Hata katika maeneo
yaliyopimwa Jijini Dar es salaam, mitandao ya maji taka haijakarabatiwa na
kupanuliwa kwa wakati kwa kuzingatia ongezeko la watu suala ambalo
lisipochuliwa kwa uzito unaostahili madhara yatatokea katika siku za usoni.
Kwa
mujibu wa ripoti ya EWURA ya mwaka 2009, viwango vya huduma za uondoaji maji
taka katika asilimia vimewekwa katika mabano Mwanza (3.1%), Moshi (5.8%) Arusha
(7.0%), Dodoma (11.6%), Tabora (1.3%) na Tanga (9.3%).
Taarifa
hiyo inaeleza kuwa kwa upande wa Dar es salaam huduma za mtandao wa maji taka
ni kwa kiwango cha asilimia 4.8 katika Jiji lenye msongamano mkubwa wa watu
ambapo hata katika kata zilizopimwa kama ya Sinza na nyinginezo hali ni tete.
Matokeo
yake ni kuwawapo wakazi ambao hukiuka sheria na kusubiri mvua zinyeshe na
kutiririsha maji taka hali ambayo ni hatari kwa afya za wananchi; kwa upande wa
vijijini unafuu unapitakana katika ukubwa wa maeneo ya kuweza kuchimba vyoo,
kinyume na mijini ambapo kadiri gharama za kukodi magari ya maji taka kwa sekta
binafsi zisizodhibitiwa zinavyozidi kuongezeka ndivyo hatari zinavyozidi katika
maeneo wanayoishi wananchi wa kipato cha chini.
Udhaifu wa kiutendaji katika miradi
ya maji inayosimamiwa na Halmashauri, kamati na jumuiya za watumia maji:
Katika
baadhi ya Halmashauri nchini ikiwemo za Jiji la Dar es salaam yamekuwepo
matumizi mabaya na udhaifu wa kiutendaji katika miradi ya maji inayosimamiwa na
Halmashauri kwa kushirikiana na kamati za maji au jumuiya za watumia maji.
Kushindwa
kushughulikiwa kwa matatizo ya kimfumo kuhusu uendeshaji wa miradi ya maji,
kutokutekelezwa kwa wakati kwa vipaumbele vya maji kwa mujibu wa bajeti za
Halmashauri iliyopitishwa na madai ya ufisadi katika miradi inayosimamiwa na
kamati za maji au jumuiya za watumiaji katika baadhi ya maeneo kumesababisha
wananchi kukosa huduma ya maji.
Hata
hivyo, pamoja na wananchi kuwasilisha malalamiko yao Wizara ya Maji na Ofisi ya
Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- TAMISEMI) ili kutimiza
wajibu wa usimamizi na ufuatiliaji hatua za haraka zimekuwa hazichukuliwi hali
inayohitaji mjadala na usimamizi wa kibunge.
Katika
mjadala utakaotokana na hoja hii, naamini wabunge wenzangu mchangia uzoefu wenu
katika maeneo mnayotoka; naomba kwa upande wangu nitoe mfano wa Manispaa ya
Kinondoni kuhusu mradi wa maji kata ya Goba.
Tatizo
la maji katika kata ya Goba limedumu sasa kwa kipindi cha miaka zaidi ya mitano, pamoja na kwamba serikali
inaowajibu kulinda maslahi ya walaji na kuhamasisha upatikanaji wa huduma ya
maji kwa watumiaji wakiwemo wa kipato cha chini na walio pembezoni au katika
mazingira magumu mamlaka zinazohusika hazijaweza kutimiza wajibu ipasavyo
kuhusu kata ya Goba.
Jitihada
nyingi zimefanywa zilizofanywa na wakazi wenyewe kama njia mbadala ya kupata
huduma hiyo muhimu kwa maisha ya Binadamu lakini zimekuwa zikikwamishwa na
baadhi ya watendaji wa Halmashauri kwa kushindwa kusimamia kwa kurejesha na
kupanua huduma hiyo muhimu kwa wananchi hata baada ya kupokea malalamiko katika
nyakati mbalimbali .
Mnaweza
mkajiuliza sababu za suala hili kuvuka mipaka ya Baraza la Madiwani wa Manispaa
ya Kinondoni, mpaka Bungeni; ni muhimu ifahamike mapema kwamba jitihada katika
ngazi hizo kwa miaka mingi hazijaweza kuleta ufumbuzi hali inayohitaji chombo
cha juu zaidi kwa niaba ya wananchi; yaani Bunge kujadili kwa kuwa Wizara ya
Maji nayo imeshindwa kuchukua hatua zinazostahili kwa wakati.
Historia
ya tatizo hili inaonesha kuwa wakazi wa
Goba wameshawahi kuandika barua kwa Waziri wa Maji barua ya tarehe 15/10/2009 ikieleza kero ya
maji kwa wananchi na wakimtaka alipatie ufumbuzi tatizo hilo na nakala ya barua
hiyo ilipelekwa kwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, na mkuu wa wilaya ya
Kinondoni pamoja na hayo bado tatizo linaendelea kutopatiwa ufumbuzi huku
wakazi wa Goba wakiendelea kukosa haki yao ya msingi kwa kuwa hakuna maisha
bila maji.
Kushindwa
kulipatia ufumbuzi tatizo hilo kulipelekea wananchi pia kuandika barua ya wazi kwa waziri mkuu mheshimiwa Mizengo
Kayanza Peter Pinda wakilalamikia mradi wa maji wa muda mrefu, pamoja na barua
hiyo hakuna jitihada kamili zilizofanyika za makusudi kuondoa tatizo hilo.
Utendaji
mbovu na usimamizi mbovu wa miradi ya maji kwa manispaa ya Kinondoni chini ya kamati za maji zilizosababisha maji
kukatwa kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2007 na 2011 ndiyo chanzo cha ukosefu wa maji kwa kipindi
chote hicho.
Katika
kipindi cha karibuni, kamati ya maji Goba baada ya kukatwa kwa maji
ilimwandikia barua mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni tarehe 30/08/2011 yenye
kumbukumbu namba G/WP/GOBA/VOL013/11 ikimuarifu Mkurugenzi kuhusu kusitishwa
kwa huduma ya Maji kwa Wananchi wa Kata ya Goba.
Katika
barua hiyo ambayo mbunge nilipatiwa
nakala yake, wananchi hao walimlalamikia mkurugenzi kwa kutozifanya kazi barua
zao wakionesha mfano barua ya tarehe 22/05/2011 na kumuomba Mkurugenzi kuchukua
hatua za haraka ili huduma ya maji irejeshwe hata hivyo Manispaa ilizembea
kuchukua hatua zinazostahili.
Mnamo
tarehe 21/03/2011, nilimwandikia barua Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni
yenye namba : KUMB:OMU/MJ/005/2011 yenye
kichwa cha barua “Hatua za Haraka zinahitajika kuhusu mradi wa Maji Goba” .
Kutokana
na hatua stahili kutochukuliwa niliandika barua nyingine kwa Mkurugenzi yenye kumb. OMU/MJ/008/2011 na kupendekeza hatua za haraka kuchukuliwa
ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha kutoka mfuko wa Jimbo Tsh 3,000,000.00
zinapelekwa haraka katika Akaunti ya
maji Goba ikiwa ni sehemu ya kuchangia katika wajibu wa manispaa za kujenga
uwezo wa mradi husika na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni
alifanya ziara Goba tarehe 31/01/2012 katika ziara ile mkurugenzi
aliwaahidi wakazi wa Goba kurejesha huduma ya Maji ndani ya wiki moja lakini
hadi sasa ni zaidi ya mwaka wananchi
bado hawajapata huduma hiyo.
Tarehe 18/03/2012
niliwaandikia barua tena DAWASA yenye kumbukumbu namba OMU/MJ/006/2012 kuhusu
hatua ambazo DAWASA imechukuakuhusu matatizo ya maji katika kata ya Goba,
katika barua hiyo nilitaka kujua hatua ambazo DAWASA imechukua kushughulikia
matatizo ya maji Goba hususani juu ya kufanya majadiliano na Manispaa ya
Kinondoni ili kuwa na mfumo endelevu
zaidi wa utoaji wa huduma ya maji katika kata ya Goba ambayo ina ongezeko kubwa
la wakazi, makazi na mahitaji mengine mengi kwa sasa.
Wizara ya Maji na mamlaka
zingine za kiserikali zinapaswa kuharakisha uchunguzi na kuchukua hatua
dhidi ya wote waliohusika kusababisha uvunjwaji wa haki za watumiaji wa huduma
ya maji, udhaifu wa usimamizi wa miradi ya maji na ukosefu wa huduma ya maji
katika kata ya Goba kwenye Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es salaam ili kutoa
fundisho kwa maeneo mengine.
Kwa kufanya hivyo, Serikali ifuatilie
mpaka Manispaa ya Kinondoni, DAWASA na DAWASCO wawezeshe huduma ya maji kurejea
kwa wananchi, kupanua kwa dharura wigo wa upatikanaji wa maji kwa wananchi wa
Kata ya Goba pamoja na kuboresha mfumo mzima wa upangaji, utekelezaji na
usimamizi wa miradi ya maji katika Manispaa ya Kinondoni, DAWASA na DAWASCO.
Aidha
ili kupata ufumbuzi wa kudumu Wizara ichukue hatua za ziada ili kata ya Goba
itoke katika kupatiwa huduma ya maji chini ya Manispaa ya Kinondoni na badala
yake ihudumiwe na DAWASA pamoja na
DAWASCO ili kuwezesha uboreshaji mpana wa miundombinu.
Mheshimiwa Spika;
Upungufu katika usimamizi wa Sheria
za maji na haja ya kuharakisha utungaji wa kanuni na marekebisho ya sheria
husika:
Hatua
kuhusu uboreshaji wa huduma ya maji safi na uondoaji wa maji taka katika Jiji
la Dar es salaam zinasimamiwa na sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge hili.
Baadhi
ya Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji ya mwaka
2009, Sheria ya maji safi na usafi wa mazingira ya mwaka 2009, sheria ya
mamlaka ya udhibiti wa nishati na maji ya mwaka 2001 na sheria ya mamlaka ya
maji safi na maji taka Dar es salaam ya mwaka 2001. Hata hivyo kumekuwa na
upungufu wa kusimamia utekelezaji wa sheria hizo ikiwemo katika kutunga kanuni
na kuchukua hatua kwa wakati.
Serikali
inapaswa kutoa maelezo bungeni ni kwanini mpaka mwezi Julai mwaka 2012 ilikuwa
haijakamilisha kutunga kanuni zinazohusu uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Uwekezaji
wa Maji (National Water Investment Fund) toka Sheria husika itungwe mwaka 2009.
Bunge lijadili hoja hii ili pamoja na mambo mengine liisimamie Serikali mfuko
huu uweze kufanya kazi kwa manufaa ya wananchi wote wenye kuhitaji uwekezaji
toka mfuko huu kuondoa matatizo ya maji nchini ikiwemo Dar es salaam.
Mheshimiwa Spika;
Aidha,
katika utekelezaji wa sheria umeonekana pia upungufu mwingine wa ziada
unaohitaji marekebisho ya sheria mbalimbali. Mfano, ukiondoa maeneo ya mijini
ambapo huduma za maji zinasimamiwa na mamlaka za maji safi na maji taka kwa
upande wa Dar es salaam ikiwa ni DAWASA; maeneo ya vijijini kote nchini
yanayohudumiwa na Halmashauri ikiwemo maeneo ya pembezoni ya Dar es salaam
yanayohudumiwa na Manispaa, mifumo ya usimamizi ina udhaifu kutokana na
upungufu wa kisheria.
Kutokana
na hali hiyo kwa nyakati mbalimbali limetolewa pendekezo na wabunge kwamba
paundwe Wakala wa Maji (TANWATER) kama ilivyo Wakala wa Barabara (TANROADS)
hata hivyo Serikali mpaka sasa haijatekeleza pendekezo hilo ambalo utekelezaji
wake utahusisha pia marekebisho ya sheria mbalimbali.
Mheshimiwa Spika;
Sheria
ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam ya mwaka 2001 nayo inahitaji
kufanyiwa marekebisho makubwa. Kati ya mambo yanayohitajika kufanyika ni pamoja
na kurekebisha ramani ya awali iliyopitishwa ikiwa ni sehemu ya sheria husika
kuhusu eneo ambalo kwa mujibu wa sheria linapaswa kuhudumiwa na DAWASA
(designed area) ili kuendana na ukuaji wa jiji pamoja na maeneo jirani ya
Kibaha na Bagamoyo.
Aidha,
marekebisho mengine yanahitajika katika utaratibu mzima wa DAWASA kutoa
mikataba kwa makampuni mengine kuendesha huduma ya maji kwa niaba yake ili
kuepusha kasoro zilizojitokeza wakati wa mkataba wa City Water na kasoro
nyingine zinazoendelea hivi sasa katika mkataba baina ya DAWASA na Kampuni ya
Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO).
Marekebisho
yanayohitajika kufanyika ni pamoja na ya kubadili muundo wa Bodi ya DAWASCO
ikiwemo kuwezesha uwakilishi wa Halmashauri za Manispaa za Dar es salaam katika
bodi ya DAWASA.
Kwa
upekee wa muundo wa Mkoa wa Dar es salaam, Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam
inafanya kazi ya uratibu tu wakati ambapo sehemu kubwa ya taratibu za ardhi,
mipango miji na ujenzi ziko katika Halmashauri. Halmashauri za Manispaa ndizo
ambazo zinahusika kwa kiwango kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji
ukiondoa ya DAWASA katika kata na mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam.
Hata
hivyo, wakati halmashauri ya Jiji la Dar es salaam inawakilishwa kati bodi ya
DAWASA, Manispaa zote tatu hazina uwakilishi hali ambayo inapunguza kiungo cha
mawasiliano na kuathiri nguvu za Halmashauri katika kufuatilia miradi ya maji
inayotekelezwa katika maeneo yao na wakati mwingine kuchelewesha miradi husika.
Marekebisho
ya sheria ya DAWASA yanapaswa kuhusisha pia kurekebisha adhabu zinazotokana na
makosa ya uharibifu wa miundombinu ya maji, wizi wa maji safi na uunganishaji
kinyemela wa mabomba ya maji taka; kwa kuwa adhabu zilizopo kiwango chake
kimepitwa na wakati na hakilingani na kukithiri kwa makosa ya biashara haramu
ya maji na hujuma katika miundombinu ya maji katika jiji la Dar es salaam.
Kasoro katika upangaji na
utekelezaji wa Mpango Maalum wa kutatua tatizo la Maji katika Jiji la Dar es
salaam:
Ikumbukwe
kuwa katika kutafuta ufumbuzi Mwezi Machi 2011 Baraza la Mawaziri lilipitisha
Mpango Maalum wa Maji Dar es salaam na Pwani wenye mgawanyo wa fedha ufuatao:
|
Mahitaji ya fedha Mpango Maalum
|
|
Na.
|
Kazi
zitakazotekelezwa
|
Gharama
2010-2013
(SH.BILIONI)
|
Makadirio kila mwaka
wa fedha (sh. bilioni)
|
|
2010/11
|
2011/12
|
2012/13
|
2013/14
|
|
1
|
Upanuzi wa mtambo wa
Ruvu Juu
|
17.25
|
0.45
|
6.00
|
6.00
|
4.80
|
|
2
|
Upanuzi wa mtambo wa
Ruvu Chini
|
122.50
|
9.38
|
24.28
|
56.98
|
31.88
|
|
3
|
Kazi ya visima vya
Kimbiji na Mpera
|
133.15
|
10.35
|
70.90
|
29.25
|
22.65
|
|
4
|
Ujenzi wa bwawa la
Kidunda
|
174.75
|
3.00
|
7.80
|
83.70
|
80.25
|
|
5
|
Upanuzi wa mtandao wa
mabomba ya maji safi
|
82.40
|
-
|
24.05
|
37.15
|
21.20
|
|
6
|
Uchimbaji na
ukarabati wa visima katika maeneo yasiyo na maji.
|
4.00
|
1.50
|
2.50
|
-
|
-
|
|
7
|
Kuimarisha utoaji wa
huduma ya maji
|
18.00
|
-
|
5.00
|
6.00
|
7.00
|
|
8
|
Kuboresha uondoaji wa
majitaka (upanuzi wa mtandao na ujenzi wa mitambo mitatu ya maji taka)
|
100.60
|
-
|
-
|
50.30
|
50.30
|
|
9
|
Miradi mingine
|
0.20
|
0.20
|
-
|
-
|
-
|
|
10
|
Elimu kwa umma
|
1.00
|
0.50
|
0.20
|
0.20
|
0.10
|
|
|
Jumla
Kuu
|
653.85
|
25.38
|
140.73
|
269.58
|
218.18
|
Katika
kutekeleza mpango huu maalum, natambua kwamba upanuzi wa mfumo wa maji wa Ruvu
Juu ikiwemo ujenzi wa wa Tanki la Kibamba na Bomba mpaka Kimara utafanyika na
fedha za ujenzi huo kiasi cha dola milioni 132 zimepatikana ikiwa sehemu ya
mkopo wa dola milioni 178 kutoka Serikali ya India. Nafahamu pia kwamba ujenzi
wa kupanua intake na machujio mapya ya maji unaendelea kwa udhamini wa Shirika
la Milenia (MCC) wa kiasi cha dola za kimarekani milioni 36.8. Naelewa pia kuwa
ujenzi wa bomba kutoka Ruvu Chini hadi Dar es Salaam utakaogharimu shilingi
bilioni 122.5 za walipa kodi wa Tanzania umeanza.
Hata
hivyo, kiwango cha uwekezaji huo hakijaweza kufikisha malengo yaliyopitishwa na
Baraza la Mawaziri na Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano uliopitishwa na Bunge
hili; kwa kuwa jumla mpaka mwaka wa fedha 2012/2013, zilipaswa kuwa zimetumika
au walau zimetengwa kiasi cha shilingi bilioni 435.67 ikiwa ni hatua ya haraka
ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka katika Jiji la
Dar es salaam na mikoa mingine inayoguswa na miradi hiyo ikiwemo ya Morogoro na
Pwani.
Mheshimiwa Spika;
Hivyo,
pengo hilo linapaswa kuzibwa kwa haraka kupitia nyongeza ya fedha katika Mpango
wa Maendeleo na Bajeti ya mwaka 2013/2014 kwa kuchukua hatua za haraka.
Serikali ieleze bungeni imefikia wapi katika kupata fedha za kulipa fidia ya
maeneo ya hifadhi ya maji ya Kimbiji na Mpera kiasi cha shilingi bilioni 27
ambayo ilipaswa kuwa imelipwa tangu mwaka 2011 na lini hasa ujenzi utaanza.
Serikali
ieleze iwapo ujenzi wa Bwawa la Kidunda Mkoani Morogoro unaokadiriwa kugharimu
shilingi bilioni 175 utaingizwa katika vipaumbele vya taifa kwa mwaka 2013/2014
kwa kuzingatia umuhimu wa bwawa hilo katika kukabiliana na athari za mabadiliko
ya tabia nchi ambayo yenye kufanya upatikanaji wa maji kutokuwa na uhakika
katika mto Ruvu kipindi chote cha mwaka na kusababisha uhaba wa maji kwa
wananchi wa Pwani na Dar es Salaam.
Hatua
hizi zote zitakuwa na tija kwa wananchi wengi zaidi iwapo zitaambatana na
ujenzi wa mfumo wa usambazaji wa maji katika maeneo ambayo hayakufikiwa katika
awamu iliyopita; maeneo ambayo wananchi huyaita ‘yaliyorukwa katika uwekezaji
wa mabomba ya mchina’ na ukarabati wa mifumo chakavu ya usambazaji wa maji.
Serikali inapaswa kueleza ni lini maeneo hayo yatawekewa mtandao wa mabomba
ambayo yanakisiwa kuhitaji jumla ya shilingi bilioni 82.4.
Mheshimiwa Spika;
Kwa
upande mwingine, ili kuondokana na ‘bomu la wakati’ serikali ione umuhimu wa
kutafuta fedha kwa haraka kiasi cha shilingi bilioni 100.6 kwa ajili ya
kuboresha huduma za maji taka kama ilivyoahidi kwa nyakati mbalimbali.
Fedha
hizi zinaonekana ni nyingi lakini ni matokeo ya udhaifu wa miaka mingi katika
mipango miji katika Jiji la Dar es salaam hali inayosababisha gharama za
usambazaji wa huduma ya maji safi na uondoaji wa maji taka kuwa kubwa. Upo
umuhimu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutambua kwamba
ongezeko la zaidi ya asilimia 70 ya maeneo ya makazi ambayo hayajapimwa katika
Jiji la Dar es Salaam ikilinganishwa na wastani wa asilimia 30 wa miji mingine
mikuu ya mikoa ni hali yenye kuathiri kwa kiwango kikubwa uchumi wa nchi na
maisha kwa wananchi kwa ujumla.
Ujenzi
wa miundombinu hiyo mipya na ukarabati wa ile chakavu ya usafirishaji hautakuwa
na maslahi tu kwa wananchi kwa kuwawezesha kupata huduma bali pia utakuwa na
tija kwa nchi kwa kupunguza upotevu wa maji mpaka asilimia 25 na hivyo
kudhibiti hasara ambayo inalikumba taifa hivi sasa kutokana na kiwango cha maji
kinachopotea kwa Jiji la Dar es Salaam pekee.
Bajeti
ndogo ya sekta ya maji na utegemezi wa fedha kutoka nje:
Mheshimiwa Spika;
Fedha
zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenye sekta ya maji ni kidogo na
hata hizo zinazotengwa utegemezi wa wahisani kutoka nje ni mkubwa kwa kiwango
cha kuathiri miradi katika Jiji la Dar es salaam na nchi kwa ujumla.
Kujibu
wa ripoti ya Hali ya Umaskini na Maendeleo ya Watu mwaka 20112 (PHDR) Fedha za
ndani za kutekeleza bajeti ya Sekta ya Maji imekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka
toka 57% katika mwaka wa fedha 2005/06 hadi 10% kwa mwaka wa fedha 2011/12.
Hali
hii imesabababisha kukithiri kwa utegemezi katika vyanzo vya mapato toka nje na
kwa wabia wa maendeleo kuwezesha miradi ya maji; fedha ambazo hazipatikani kwa
wakati na kwa kiwango kinachokidhi mahitaji.
Kwa
mwaka 2011/12 tumeshuhudia kutokutimizwa kwa azimio la serikali la kutenga
kiasi cha Dola za Kimarekani 128 milioni kutekeleza Programu ya Kuendeleza
Sekta ya Maji (WSDP) huku bajeti pangwa ikiwa ni dola za kimarekani 28 milioni
tu kwa mwaka huo 2011/12.
Tufahamu
kwamba kupungua huku kwa kiwango cha bajeti katika sekta ya maji kunapingana
hata na azimio la Sharm el Sheikh la nchi za Umoja wa Afrika la mwaka 2008 la
kutaka dhamira na azma ya kuongeza kipaumbele cha kisiasa katika utengwaji na
kuwekwa wazi kwa bajeti kwa ajili ya sekta ya maji safi na maji taka.
Mheshimiwa Spika;
Utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2012/2013 umeendelea kuonesha
upungufu katika utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo katika sekta ya maji,
taarifa zinaonyesha kwamba katika kipindi cha miezi sita ya kwanza Jumla ya
Shilingi Bilioni 29 tu ndizo zilitolewa ikiwa ni sawa na asilimia 36 katika
fedha za ndani. Hali hii ni kidogo ikizingatiwa kiwango kilichoidhinishwa na
tume ya mipango kikiwa ni shilingi 48,326,792,184 kwa kipindi cha robo ya
kwanza pekee.
Mheshimiwa Spika,
Mapungufu yanayojitokeza katika utekelezaji wa mipango ya serikali
hususani katika ugawaji wa rasilimali fedha ambazo zimeidhinishwa na bunge
katika huduma muhimu za jamii kama maji, matokeo yake ni kuwa na huduma mbovu,
hivyo napendekeza bunge lijadili hali hiyo na kupitisha hatua za haraka ambazo
zitanufaisha nchi kwa ujumla ikiwemo Jiji la Dar es Salaam.
Hatua
hizo zitawezesha fedha za miradi ya
maendeleo ya maji kutolewa kwa wakati katika miezi iliyobaki ya mwaka wa fedha
2012/2013 na kupewa kipaumbele katika Mpango wa Mwaka wa Maendeleo na Bajeti
kwa mwaka 2013/2014.
Mheshimiwa Spika;
Udhaifu katika utekelezaji wa
Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini:
Tangu
mwaka 2000 Bunge hili limekuwa likipewa ahadi za utekelezaji wa Programu ya
Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RWSSP). Wakati maelezo ya kuanza kwa
mpango huo yalipoletwa bungeni mwaka 2003, wakati huo ukiitwa mpango wa vijiji
kumi (quick wins), yapo maeneo katika Jiji la Dar es salaam ambayo yalikuwa na
vijiji na yaliingizwa katika mpango huo. Hata hivyo, mpaka leo miaka takribani
kumi baadaye mwaka 2013 maeneo hayo yakiwa yameshapanda hadhi na kuwa mitaa
miradi hiyo haijatekelezwa kwa ukamilifu wake.
Maeneo
hayo yamekosa maji kwa pande zote, hayajahudumiwa na DAWASA na DAWASCO kwa kuwa
yapo kwenye vijiji kumi; na mradi huo wa vijiji kumi haujaweza kuwafanya
wananchi hao wapate huduma ya maji.
Hali
hii haihusu Halmashauri za Manispaa za Jiji la Dar es Salaam za Ilala,
Kinondoni na Temeke; inahusu halmashauri zote nchini ambazo mpango huo ulipaswa
kutekelezwa. Naamini kujadiliwa kwa hoja hii kutawezesha wabunge wenzangu
kueleza pia uzoefu katika maeneo yenu ya vijijini na mijini hatimaye kutokana
na mapendekezo ya hoja hii; Bunge likapitisha maazimio ambayo yataweza
kuchangia katika kurekebisha hali hii.
Mheshimiwa Spika;
Programu
hii ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ilipaswa kutekelezwa kwa awamu nne,
ambapo utekelezaji wa awamu ya kwanza baada ya kucheleweshwa toka mwaka 2003
ulipaswa kuanza mwaka 2005/2006 na kukamilika mwaka 2010/2011. Kwa maneno rahisi
ni kwamba hadi kufikia hivi sasa ilipaswa tayari maji yawe yameshapatikana
katika vijiji kumi vya kila halmashauri nchini, hata hivyo ukomo wa muda wa
awali ukiwa umeshapita kwa zaidi ya mwaka mmoja; utekelezaji katika maeneo
mbalimbali nchini haukufanyika hata robo.
Hali
iko hivyo, wakati ambapo fedha zimetumika bila maji kupatikana; katika hatua
hiyo ya kwanza jumla ya shilingi bilioni 96.4 zimetumika kwenye “quick wins”
hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka 2012 huku maji kwa sehemu kubwa kukiwa hakuna;
hali ambayo ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Mheshimiwa Spika;
Katika
ufuatiliaji wangu kuhusu masuala ya maji katika Manispaa za Jiji la Dar es
salaam, katika halmashauri zingine na katika Wizara ya Maji nimebaini kwamba
hali hiyo ilisababishwa na mikataba mibovu yenye dalili za ufisadi, kukosekana
kwa uwajibikaji miongoni mwa makampuni yaliyopewa zabuni katika mazingira ya
utata na udhaifu katika mchakato mzima wa zabuni na usimamizi wa miradi.
Matokeo
yake watafiti na wachimbaji binafsi wengi wao wakiwa hawana uwezo wa vifaa na
wataalamu walipewa kazi na kulipwa fedha bila hata ya mchakato kukamilika;
badala ya kuwekwa mfumo wa watafiti kuhusika pia na uchimbaji na kulipwa kwa
kadiri na matokeo na hatua iliyofikiwa. Anafanya utafiti mwingine, anachukua
fedha zake anakwenda; anayekwenda kufanya uchunguzi ni mwingine naye anachukua
fedha zake anakwenda; anayejenga miundombinu ni mwingine, naye anaelekezwa eneo
na baadaye kueleza kwamba hakuna maji huku hasara ikiwa imeshapatikana.
Ripoti
ya Tathmini (Appraisal Report) ya Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira
Vijijini (Rural Water Supply and Sanitation Program) ya mwaka 2010 inaonyesha namna ambavyo
awamu ya kwanza katika ya mwaka 2007 mpaka 2010 ilivyoshindwa kutekelezwa kwa
ufanisi. Usimamizi wa kutosha wa kibunge unahitajika kuhakikisha awamu ya pili
(RSSWP Phase II), ambayo awali ilipangwa ifanyike kuanzia mwaka 2011 mpaka 2014
inafanyika kwa kuanzia na kufanya ukaguzi wa awamu iliyopita.
Bunge
lako lijadili hali hii na kupitisha maazimio yenye kuwezesha ukaguzi maalum
ufanyike kwenye matumizi ya bilioni 96.4 za mradi wa maji safi na mazingira
vijijini katika Jiji la Dar es salaam na Halmashauri zote nchini ili
kasoro hizo zisijirudie katika awamu ya
pili ya programu hiyo inayotarajiwa kuanza mwezi Juni mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika;
Baada
ya maelezo hayo sasa naomba kuwasilisha hoja kwa mujibu wa kanuni ya 54 fasili
ya (1) (2) na (3) ya kupendekeza bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua
za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji
taka katika Jiji la Dar es salaam.
MABADILIKO
KATIKA HOJA KUHUSU HATUA ZA HARAKA ZA
KUBORESHA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA USHUGHULIKIAJI WA MAJI TAKA KATIKA JIJI
LA DAR ES SALAAM
(Kwa
mujibu wa Kanuni 55 (10) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge)
Kwa kuondoa maneno
kuanzia “KWA KUWA, kati ya mwaka 2003….. (yaliyo kuanzia katika ukurasa wa 42
na kuendelea mpaka ukurasa wa 45 yanapoishia maneno maneno)…….. mapendekezo ya
mpango wa taifa”
Na kuingiza maneno:
“KWA
KUWA, Programu ya Maji Safi na Mazingira Vijijini ikiwemo katika Manispaa za
Jiji la Dar es Salaam ilipaswa kutekelezwa kuanzia mwaka 2005/2006 na
kukamilika mwaka 2010/2011 kwa kugharimu dola za kimarekani milioni 292 hata
hivyo tathmini ya miaka miwili na nusu ya utekelezaji (mid term review)
imebanisha kasoro nyingi katika utekelezaji.
KWA
KUWA, Kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na
upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo
ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP)
uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao
wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji huku kukiwa na upungufu katika
uzalishaji, upotevu wakati wa usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma
za ufisadi katika matumizi.
NA
KWA KUWA, Wizara ya Maji iliandaa waraka maalum wa kuiomba Serikali kutenga
kiasi cha shilingi bilioni 653.85 Mpango Maalum 2011-2013 wa kuboresha huduma
za majisafi na uondaji wa majitaka katika Jiji la Dar es salaam na kupitishwa
na Baraza la Mawaziri mwezi Machi 2011 lakini utekelezaji wake unaelekea
kucheleweshwa mpaka mwaka 2016.
NA
KWA KUWA , katika mwaka wa fedha 2011/2012 na 2012/13 Serikali haikutenga
kiwango kamili cha fedha kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka
Mitano ulioidhinishwa na Bunge na kwa kuzingatia mgawanyo wa Mpango Maalum wa
Maji Safi na Maji Taka katika Jiji la Dar Es Salaam na kauli ya Serikali ya
tarehe 7 Novemba 2012.
NA
KWA KUWA, kwa mujibu wa ibara ya 62 (2)
na (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ,
Bunge ndicho chombo kikuu chenye madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na
kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu.
NA
KWA KUWA, kwa mujibu wa ibara ya 63(3) katika utekelezaji wa madaraka yake
bunge laweza kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda
mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
kutunga sheria pale utekelezaji unapohitaji kuwapo sheria.
NA
KWA KUWA, Malengo ya
Kitaifa yalikuwa ni kuwapatia wakazi wa Mjini maji kwa asilimia 90 ifikapo
mwaka 2010 na kwamba malengo hayo kwa Jiji la Dar es Salaam yamesogezwa mbele
na kuwekwa malengo mapya ya upatikanaji wa huduma ya maji safi kufikia asilimia
90 na uondoaji wa maji taka kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2015.
KWA HIYO BASI,
Bunge linaazimia kwamba Serikali ichukue hatua za haraka zaidi za kuboresha
upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es
salaam:
NA KWAMBA,
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi maalum wa matumuzi ya fedha matumizi ya
bilioni 96.4 za mradi wa maji safi na mazingira vijijini katika Jiji la Dar es
salaam na Halmashauri zingine na kuwezesha hatua za ziada kuchukuliwa.
NA KWAMBA,
Kufuatia kauli iliyotolewa bungeni tarehe 7 Novemba 2012 kuhusu Mpango Maalum
wa kutatua tatizo la maji katika Jiji la Dar es salaam uliopitishwa mwezi Machi
2011 Serikali izingatie makisio ya awali ya gharama za mpango huo na kuingiza
mahitaji yaliyobaki kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mwaka 2013/2014 na
Bajeti ya mwaka 2013/2014.
NA
KWAMBA, Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na
Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni 2010 unaohusisha
uchimbaji wa visima 29 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 uwekewe muda wa ukomo
wa kukamilika kwa dharura katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi
sasa ikiwemo iliyozinduliwa Oktoba 2012 yenye kuhitaji miundombinu ya ziada
kufikia wananchi zaidi.
NA
KWAMBA, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa thamani
ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa ukarabati na upanuzi wa
miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo
na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) kwa kurejea
ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard
Humphreys.
NA
KWAMBA, EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi (performance audit) wa miradi ya
visima vya maji takribani 200 ambavyo vilichimbwa na serikali na kukabidhiwa
kwa DAWASCO, jumuiya za wananchi na taasisi mbalimbali lakini haitoi huduma
inavyostahili kwa kadiri ya malengo ya awali.
NA
KWAMBA, EWURA iharakishe kukamilisha mchakato ulioanza wa kutunga kanuni za
udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa upande wa sekta binafsi katika
Jiji la Dar es salaam.
NA
KWAMBA, Kamati husika ya Bunge ijadili taarifa ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu
usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini (performance audit
report on the management of water distribution in urban areas) ya Januari 2012
ili maoni na mapendekezo yazingatiwe wakati wa kujadili na kushauri kuhusu
mapendekezo ya mpango wa taifa na bajeti ya nchi.
NA
KWAMBA, Serikali iwasilishe bungeni haraka iwezekanavyo muswada wa sheria ya
marekebisho ya sheria mbalimbali za majisafi na majitaka (Water Supply and
Sanitation Miscellaneous Amendment Bill) ili kushughulikia upungufu
uliojitokeza katika utekelezaji wa sheria zilizopo na kuweka mfumo thabiti wa
usimamizi wa sekta ya maji nchini.”
Naomba
kuwasilisha.
…………………
John
John Mnyika(Mb)
Jimbo
la Uchaguzi-Ubungo