Thursday, April 26, 2012

"MAUAJI YA HALAIKI" ya Watoto wa Tanzania kupitia... 25/04/2012


 

 
mauaji ya halaiki senkoro F.E.M.K Senkoro

Makala kwa Ajili ya Warsha ya Usambazaji wa Matokeo ya Tafiti Kuhusu Kuhusu Lugha ya Kufundishia Sekondari na Vyuoni Tanzania Desemba 5, 2006 F.E.M.K. Senkoro Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Kwanza kabisa, nieleze matukio mawili ambayo nimekutana nayo hapahapa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Asubuhi moja nilikutana na mwanafunzi wangu mmoja akiwa anatoka jasho chapwachapwa mwili mzima. Kwa vile yalikuwa majira ya baridi hapa Dar es Salaam, nilimwuliza kama anaumwa. Alinijibu kuwa hakuwa anaumwa, bali alikuwa na uhudhurishaji wa swali la semina siku hiyo. Kidogo alinishangaza kwani katika semina zangu na hata katika mitihani yangu alikuwa akifanya vizuri sana. Sikuelewa kwa nini alikuwa anaogopa semina ile hadi aliposema, "Afadhali semina yenyewe ingelikuwa ya Kiswahili. Hii ni kwa Kiingereza, na sijalala usiku kucha, na hata chamshakinywa kimenishinda asubuhi hii. Unajua Profesa, si kwamba mawazo sina, ila siwezi kuyatoa vizuri kwa Kiingereza, na siwezi hata kuonyesha hisia zangu kikamilifu kwa lugha hiyo. Basi tu. " Nilidhani anatania, lakini nilipomwangalia usoni nilijua kuwa hakuwa anatania hata kidogo. Niliamua kuwauliza wanafunzi mbalimbali kuhusu hali hiyo, na karibu wote wakanijibu kuwa hali ile huwapata kila wanapokabiliwa na zoezi la kuhudhurisha kwa Kiingereza katika semina. Na hawa hawakuwa wa mwaka wa kwanza tu, bali hadi wa mwaka wa nne wote walilalamikia hali hiyo.

Tukio la pili lilinitokea hivi karibuni sana nilipokaribishwa na mwalimu mwenzangu kwenda kutoa muhadhara kuhusu ngano ambazo zinavuka mipaka ya kijiografia na kiutamaduni. Muhadhara huu ulikuwa kwa Kiswahili. Na mwishoni niliwaeleza wanafunzi kuwa nilikuwa na kifikirishi kuhusu mada ile na kwamba ningempatia mwakilishi wa darasa kitini hicho. Nilipowaeleza tu kuwa kifikirishi chenyewe kilikuwa kwa lugha ya Kiingereza, wanafunzi wote waliguna na kuonyesha kukata tamaa. Walionyesha dhahiri kuwa kifikirishi cha Kiingereza kisingewafikirisha kwani wasingeambulia kitu.

No comments:

Post a Comment