Monday, April 30, 2012

Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aeshi Hillary avuliwa Ubunge na Mahakama


 
Mussa Mwangoka, Sumbawanga
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Sumbawanga imetengua Ubunge wa Aeshi Hilaly (Sumbawanga Mjini- CCM) kuanzia jana.Hukumu hiyo ya kurasa 68, iliyosomwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Betwell Mmila na kuchukua saa tatu, imekuja siku chache baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kumvua Ubunge Godbless Lema (Arusha Mjini- Chadema).

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mmilla alisema kati ya hoja 21 zilizowekewa pingamizi na aliyekuwa mgombea ubunge kupitia Chadema, Nobert Yamsebo ni vipengele viwili pekee ambavyo mahakama hiyo imeridhia kuwa vina dosari katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 31, 2010.

Alivitaja vipengele ambavyo vilikuwa na dosari kuwa ni pamoja na kuwepo kwa mazingira ya rushwa katika uchaguzi na kutokuwapo kwa mazingira huru katika kampeni kwenye baadhi ya maeneo ya jimbo hilo.

Jaji Mmila alisema aliyekuwa mgombea wa CCM (Hilaly), alikwenda kwenye kikao cha ndani kilichodaiwa kuitishwa na viongozi wa CCM katika eneo Shule ya Msingi Kantalamba Mazoezi na kuwashawishi baadhi ya wapiga kura kwa kuwapa rushwa ya Sh15,000 na watu wapatao sita walikuwapo kwenye mkutano huo kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.

Eneo jingine ambalo lilitajwa kuwa na dosari ni kutokuwapo kwa mazingira huru katika mchakato wa kampeni kwenye Vijiji vya Mtimbwa na Kisumba ambako mgombea wa Chadema alizuiwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo kufanya kampeni zake baada ya kumfanyia fujo.

Aidha, hukumu ya Mahakama  hiyo imemtaka Hilaly kulipa gharama zote za kesi hiyo.

Pamoja na hukumu hiyo, Mahakama hiyo imetoa fursa kwa upande wa mlalamikiwa kukata rufaa iwapo atakuwa hajaridhika na hukumu iliyotolewa.

Katika hoja ya msingi, mlalamikaji aliiomba Mahakama kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo kwa madai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu mbalimbali za uchaguzi.
Walalamikiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Msimamizi Msaidizi na Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi.

Katika kesi hiyo, mlalamikaji Yamsebo aliwakilishwa na kampuni ya kisheria ya Mkumbe Advocate and Company Ltd ya Mbeya huku upande wa Serikali ukiwakilishwa na wanasheria wawili wa Serikali, wakiongozwa na Wakili  Mkuu wa Serikali, Paul Shahidi.

Mlalamikiwa aliwakilishwa na jopo la Mawakili watatu, Juma Nassoro kutoka Kampuni ya Nassoro Advocate, Abubakar Salim wa Kampuni ya BLC Advocate na Ileth Mawalla kutoka S. Mawalla Law Consultant and Attorney ya Sumbawanga.

Baada ya hukumu

Huku hiyo ilivuta hisia za wakazi wengi wa Mji wa Sumbawanga na vitongoji vyake na baada ya kutolewa, vijana wa Chadema walianza kushangilia baada ya kufahamu kwamba Mahakama imetengua ubunge huo.

Hata hivyo, Wakili Nassoro alisema mteja wake anakusudia kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo baada ya kutathmini mwenendo mzima wa kesi hiyo.

Kwa upande wake, Yamsebo alisema kilio cha wanyonge kimesikika na Mahakama imetenda haki hali ambayo inawafanya wananchi kuendelea kuwa na imani na mhimili huo wa dola.

Katika matokeo ya uchaguzi huo yaliyotenguliwa, Hilaly  alishinda kwa kura 17,328 dhidi ya Yamsebo aliyepata kura 17,132.

Nje ya ukumbi wa Mahakama, wafausi wa Chadema walipiga kelele za furaha na kushangilia hali iliyomlazimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage kuchukua kipaza sauti na kuwataka kutulia.

Mashabiki hao wa Chadema walitii amri hiyo lakini kwa kutoka nje ya geti la kuingilia mahakamani na kuendelea kushangilia. Waliendelea kushangilia kwa kupita katika mitaa kadhaa ya mjini hapa.

Uchaguzi huo ulikuwa wa kwanza kwa Hilaly kuingia bungeni mwaka 2010. Kijana huyo alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Jangwani Sumbawanga kuanzia mwaka 1983 hadi 1989.

Chadema chatoa tamko

Baada ya kupata taarifa za hukumu hiyo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika aliitisha mkutano wa waandishi wa habari Ofisi za chama hicho, Kinondoni, Dar es Salaam na kusema sasa kinasubiri Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kutangaza tarehe ya uchaguzi.

“Tunachosubiri ni tume tu itangaze tarehe ya uchaguzi ili mgombea wetu ambaye hakutangazwa tu katika uchaguzi ule akatangazwe mshindi” alisema Mnyika na kuongeza:

“Katika uchaguzi ule mgombea wetu hakutangazwa tu, lakini kati ya majimbo tuliyoyataraji ni pamoja na Sumbawanga Mjini. Ndiyo maana mgombea wetu alifungua kesi nasi tukaunga mkono hatua hiyo kwa sababu tulijua haki haikutendeka.

No comments:

Post a Comment