WATUPA MPANGO WAKE WA MAENDELEO, PIA WAJIPANGA KUKWAMISHA BAJETI, CHADEMA WAANDAA MAANDAMANO
Daniel Mjema, Dodoma na Editha Majura, Dar
KITENDO
cha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kushindwa kuzungumzia shinikizo la
baadhi ya wabunge kutaka mawaziri wanane wajiuzulu, kimeonekana kuwakera
wawakilishi hao ambao sasa wameamua kuibana Serikali huku wakiapa
kukwamisha bajeti za mawaziri hao katika Bunge lijalo la Bajeti.
Jana
walianza kuonyesha makali baada ya kukataa mapendekezo ya Mfumo wa
Mpango wa Mabadiliko wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/2013 wakisema
hauna jipya na umetayarishwa kwa mfumo uleule kwa miaka 15 mfululizo.
Juzi,
Pinda aliahirisha Bunge bila kugusia shinikizo la wabunge hao kutaka
Serikali iwawajibishe Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo; Waziri wa Nishati
na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu; Waziri wa
Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk Hadji Mponda; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne
Maghembe; Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika.
Wakizungumza na
kwa nyakati tofauti jana, wabunge hao, wengi wao wakiwa ni wa CCM,
walisema silaha pekee waliyobaki nayo ni kukwamisha Bajeti ya Serikali
kwa mwaka 2012/2013 katika kikao kijacho cha Bunge.
Wabunge hao
pia wameonya kwamba kutojiuzulu kwa mawaziri hao kutaiweka CCM njia
panda katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwani hoja ya ufisadi ndiyo
iliyowafanya wenzao wengi wasirudi bungeni.
“Silaha kubwa
tuliyobaki nayo sasa ni kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu na
nakuambia kama ile karatasi ingerudi upya leo idadi ya wabunge wa CCM
ambao wangetia saini ingetikisa nchi,” alisema James Lembeli wa Kahama
(CCM).
Lembeli alisema anashangaa kuona mawaziri waliotakiwa
kujipima wenyewe na kuandika barua za kujiuzulu wakigoma kufanya hivyo
na Serikali kupuuza hoja hiyo akisema, hatashangaa kuona Watanzania
wakiingia mitaani.
“Kitendo cha Waziri Mkuu kutosema chochote
kuhusu kujiuzulu kwa mawaziri hao wakati akihitimisha Bunge ni kuiingiza
nchi kwenye mgogoro mkubwa. Serikali ifahamu kuwa, ipo madarakani kwa
ridhaa ya wananchi,” alisema.
Lembeli alisema wananchi walipokea
kwa shangwe taarifa ya mawaziri hao kutakiwa kujiuzulu lakini, kitendo
cha Waziri Mkuu kuwaacha na kuikwepa hoja hiyo alipokuwa akiahirisha
Mkutano wa Bunge juzi, kitaongeza chuki ya wananchi dhidi ya Serikali
yao kwa kuwa wataamini inawakumbatia mafisadi.
“Inakuwaje hawa
mawaziri wanane tu watake kuitumbukiza nchi kwenye machafuko? Uwaziri ni
dhamana aangalie huko kwenye vijiwe na mitaani watu walivyoshangilia
kusikia wametakiwa kujiuzulu leo wanagoma, unamgomea nani?” alihoji
Lembeli.
Lembeli alisema anaamini Rais atafanya uamuzi mgumu na wa
haraka kabla ya Bunge la Bajeti vinginevyo Waziri Mkulo na mawaziri
wengine watakuwa na wakati mgumu ambao haujawahi kuonekana katika
kupitisha bajeti za wizara zao.
Mbunge mmoja wa Viti Maalumu kwa
tiketi ya CCM kutoka Kanda ya Ziwa, alisema ukimya wa Rais Kikwete na
kiburi cha mawaziri wake wenye tuhuma za kweli kugoma kujiuzulu,
kumezidi kukifanya chama hicho tawala kuporomoka umaarufu.
Mbunge
wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alisema Rais Kikwete anapaswa
kuheshimu maoni na maelekezo ya wabunge na kusema hata kutaka mawaziri
wajiuzulu ni utaratibu tu wa kistaarabu.
“Sisi Wabunge 76 tuliosaini
hoja ya kutaka Waziri Mkuu ang’oke tumejitoa sadaka kwa maslahi ya nchi
lakini naamini wakati wa kumpigia kura Waziri Mkuu, wengi zaidi
watatuunga mkono kwa jinsi walivyokerwa na jambo hili,” alisema.
“Bunge
safari hii limeisha kimyakimya, Spika alipowahoji wanaoafiki hoja ya
Waziri Mkuu ya kuliahirisha Bunge waliosema siyo ndiyo waliokuwa wengi
na kama ulifuatilia Bunge lilikuwa kimya si kawaida… Rais anatakiwa
alione hilo,” alisema.
Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azzan (CCM),
alisema amesikitishwa na hatua ya mawaziri hao kugoma kujiuzulu na
kwamba kwa hali ilivyo, busara ya kawaida inataka mawaziri hao
wajiuzulu.
“Kwa busara ya kawaida wote wanaotuhumiwa kwa wizara
zao kufanya madudu wangeacha uroho wa madaraka na kujiuzulu ili kuitikia
kilio cha wabunge na Watanzania kwa sababu upepo huko nje sio mzuri
hata kidogo,” alisema Azzan.
Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM)
alisema taifa limeghafilika kwa sababu wananchi wengi nchi nzima walikaa
kwenye luninga na kusikiliza redio juzi jioni wakitarajia Waziri Mkuu
angetamka moja kwa moja kuwang’oa mawaziri hao.
“Jana kwenye baa
na vijiwe ilikuwa kama vile kuna mechi ya kukata na shoka... kwa jinsi
idadi kubwa ya wananchi walivyofuatilia hotuba ya Waziri Mkuu lakini
mwisho wa siku akawaacha solemba,” alisema.
Nape, Mukama
Baadhi
ya wabunge wa CCM waliosaini barua ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu
wamedai kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Wilson Mukama amewatisha.
Kanji
Lugola wa Mwibara alidai jana kwamba usiku wa kuamkia Jumapili, siku
moja baada ya kusaini hati hiyo alipokea simu kutoka kwa Mukama
akimtolea maneno makali kutokana na hatua yake hiyo.
“Alizungumza
maneno mengi ya vitisho kwa mfululizo bila hata kunipa nafasi ya
kujieleza, akasema, ‘nakuja huko wewe na huyo mwenzako mliosaini
mtanitambua,’ kuona hivyo tukaondoka Dodoma usiku huohuo,” Lugola
alieleza.
Alisema walisafiri hadi Dar es Salaam na kwamba
walihudhuria kikao cha Bunge cha Jumatatu iliyopita wakitokea
mafichoni.Alipotakiwa kuthibitisha madai hayo Mukama alisema: “Siwezi
kutoa habari kwa simu.”
Alipopigiwa tena na kuombwa afuatwe
ofisini alisema, “Kwa leo haitawezekana maana niko njiani natokea Dodoma
sasa hivi nimefika Gairo, kama unaweza njoo kesho.”
Lugola
alidai wakati akipokea vitisho hivyo kutoka kwa Mukama waliokuwa
wamesaini kwa upande wa CCM walikuwa yeye na Filikunjombe, baadaye
alifuatia na Nimrod Mkono.
“Kinachofanya tufikie hatua hii ni
kutoridhishwa na dhamira ya dhati ya chama chetu katika kuisafisha
Serikali… na ieleweke kuwa hatuna mpango wa kuhama chama chetu kwa kuwa
lengo letu ni kukiimarisha,” alisema.
Akizungumzia madai hayo ya
vitisho, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye alisema wabunge
hao hawana hatia kwani msimamo wao ni sehemu ya kutekeleza wajibu wao.
Alisema
ingawa hakuwa na taarifa za vitisho dhidi ya wabunge hao, CCM
hakijafanya kikao chochote kuzungumzia suala hilo na kusema kama kuna
mtu aliyewatisha basi amechukua hatua zake binafsi.
“Wabunge wana
haki ya kuhoji utendaji wa Serikali yao na hata kuiwajibisha, hakuna
mwenye haki ya kuwabagua kiitikadi, kiimani wala kikabila hivyo
wanaojadili suala hili kwa misingi ya kibaguzi hawawatendei haki…,
wanataka watekeleze vipi majukumu yao?”
Alisisitiza kuwa ndiye
msemaji wa CCM hivyo ieleweke kuwa kilichofanywa na wabunge si uasi na
jamii isiwagawe kwa namna yoyote ile bali, matendo yao ndani ya Bunge
yaheshimike kwa mujibu nyadhifa zao.
Waanza kuonyesha makali
Wabunge
waliyakataa mapendekezo ya Mfumo wa Mpango wa Mabadiliko wa Maendeleo
wa Taifa kwa mwaka 2012/2013 wakisema hauna jipya na umetayarishwa kwa
mfumo uleule kwa miaka 15 mfululizo na kwamba vigezo vyote, uchumi wa
Tanzania unakuwa kwa viwango visivyoridhisha na ukuaji huo hauendi
sambamba na kasi ya kupunguza umasikini na kukuza pato la mwananchi wa
kawaida.
Mpango huo ulioandaliwa na Tume ya Mipango kwa
kushirikiana na Wizara ya Fedha uliwasilishwa jana kwenye Kamati ya
Mipango ya Bunge na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu),
Stephen Wassira.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Fedha
na Uchumi, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Abdallah Kigoda alisema mfumo
huo unahitaji mabadiliko ili uendane na wakati uliopo ikiwamo kutoa
majibu ya tatizo la mfumuko wa bei.
“Mapendekezo yanayotayarishwa
yanajikita zaidi kwenye eneo la maelekezo badala ya maagizo. Lazima
Serikali itoe majibu kuwa sera za fedha na kodi zinatakiwa ziweje ili
kujibu tatizo la mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya shilingi.”
alisema Dk Kigoda.
Mbunge huyo wa Handeni (CCM), alisema
mapendekezo hayo hayajaeleza kwa kina namna sekta ya fedha
itakavyosaidia katika kutatua tatizo la uhaba mkubwa wa mitaji
unaohitajika kusaidia kukuza uchumi wa Tanzania.
“Hivi sasa
tunazo takriban benki 45 na taasisi kadhaa za fedha lakini bado wananchi
wengi hawajapata fursa ya kutumia huduma za kifedha katika shughuli zao
za kuibua mapato yao na kupata ajira,” alisema.
Katika
mapendekezo hayo ya kamati, Dk Kigoda alitaka kutumika kwa sheria mpya
ya madini, kampuni za simu zitozwe kodi kama inavyofanyika katika nchi
nyingine za Afrika na kodi za majengo.
Alisema mpango huo
ulipaswa kujikita katika kuagiza namna ya kudhibiti matumizi mabaya ya
fedha katika halmashauri nyingi na ubainishe usimamizi wa fedha na
kuagiza ni hatua gani zichukuliwe ili kupunguza matumizi mabaya ya
fedha.
Wabunge walichangia mpango huo waliupinga. Mbunge wa Nkasi
Kaskazini (CCM), Ally Kessy alisema anapata hofu ya taifa kujikuta
likiomba fedha za misaada kutoka nchi ya Cameroon kwa kushindwa
kukusanya kodi.
Alishangaa Serikali katika mpango huo kuelezea
kuongeza uzalishaji wa matunda wakati haina uwezo wala kuzalisha matunda
huku akiponda hoja ya kwamba itaimarisha viwanda wakati yenyewe ndiyo
iliyoviua.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu,
aliishangaa Serikali kujivunia kuwa nchi ina amani na usalama wakati
haina usalama kutokana na watu kuwa na njaa... “Hakuna vita mbaya kama
taifa kuwa na watu wenye njaa. Tatizo la mfumuko wa bei hasa katika
vyakula ni kubwa kutokana na kutokuwepo kwa uthibiti wa bei hizo.”
Akiwasilisha
mpango huo, Wassira alitaja baadhi ya maeneo ya kipaumbele kwa mwaka
2012/2013 kuwa ni miundombinu, uzalishaji na usambazaji umeme, barabara,
kilimo, viwanda, utalii, huduma za kifedha na tekinolojia ya habari na
mawasiliano.
Wassira alisema ili kupunguza pengo katika bajeti ya
maendeleo na pia kuchochea kasi ya utekelezaji wa mpango wa mwaka na
kutekeleza miradi ya kimkakati, itailazimu Serikali kukopa mikopo
maalumu kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.
Kwa kuanzia katika
mwaka wa fedha wa 2012/2013, Serikali itahitaji kukopa Dola za Marekani
540 milioni sawa na Sh864 bilioni mahsusi kwa ajili ya kusaidia
uwekezaji wa kimkakati kwa sekta binafsi ili iweze kuwekeza katika
miradi ya maendeleo.
Zitto: Sasa tunajipanga
Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe amesema baada ya Pinda kugoma
kuwachukulia hatua mawaziri hao, chama chake sasa kinajipanga kufanya
mazungumzo na vyama vyote ambavyo wabunge wake walitia saini kukubaliana
na hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu huyo ili waone namna ya
kuitisha maandamano nchi nzima.
“Lazima Watanzania waelewe suala
la kutaka mawaziri hawa wajiuzulu si la Wabunge wa Chadema wala la
Zitto, hili ni la wabunge wote isipokuwa UDP na nyinyi ni mashahidi kuwa
waliopiga kelele sana ni wabunge wa CCM. Sasa tunafanya mazungumzo na
vyama vilivyounga mkono hoja hiyo ili tupange kwa pamoja ni kwa namna
gani maandamano hayo yanapaswa kufanywa,” alisema na kuongeza:
“Tunataka
kumwambia Rais Kikwete kuwa gharika inakuja na asitafute mchawi ni ama
awaondoe mawaziri wanaotuhumiwa kwa ufisadi na utendaji mbovu au
wakumbane na Tsunami ya nguvu ya umma.
source:mwananchi
No comments:
Post a Comment