Saturday, May 5, 2012

BAADHI YA WABUNGE WAPINGA UTEUZI WA KIKWETE

SAA chache baada ya Rais Kikwete kutangaza Baraza jipya, baadhi ya wabunge wametoa maoni wakiunga mkono na wengine wakipinga uteuzi huo.

Baadhi walishauri kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi ya mawaziri waliobaki na waliong’olewa madarakani ambao taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliwataja kuhusika na ubadhirifu.

Mbunge wa Kasulu Kusini, David Kafulila, alieleza kufurahishwa kwake na Rais kubadilisha mawaziri na kuondoa watuhumiwa wakuu, lakini hakupenda kuona wengine walionyooshewa vidole na wabunge kwa ubadhirifu wakiachwa.

“Sijaridhishwa na mpangilio wa baadhi ya mawaziri. Kuachwa kwa Mkuchika nako ni tatizo kwa sababu alikotoka aliharibu. Mtu kama January Makamba angepelekwa Madini na Masele angekuwa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia. Mpango huo angalau ungesaidia wananchi kimaendeleo”.

Kafulila alipinga kuundwa kwa wizara isiyo maalumu kwa maelezo kuwa imelenga kuongeza gharama. Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe alipinga kuachwa kwa Mkuchika.

“Huyu ameboronga Tamisemi na leo anapelekwa Utawala Bora ataweza nini? Naheshimu uteuzi wa Rais lakini kwa kurudisha waliotuhumiwa kwa ubadhirifu na utendaji mbovu simuungi mkono na sifurahii”.

Akizungumzia kuondolewa kwa Mkullo, Filikunjombe alisema hiyo ni faraja ya kila Mtanzania.

“Niko safarini na sijasikiliza uteuzi, lakini nimepata taarifa kuhusu kuendelea kwa mawaziri waliopigiwa kelele kama vile Mkuchika, hapo kuna tatizo”.

Mbunge wa Mbozi Mashariki, Geodfrey Zambi, alieleza kufurahishwa na uteuzi huo ingawa alinung’unikia kuendelea kwa baadhi ya mawaziri waliokuwa wamelalamikiwa na wabunge.

“Rais amefanya mabadiliko, sipingani naye kwa sababu ameangalia msingi unaotakiwa kuwa anaoteua ni wabunge.

Alioona wanamfaa amewapa nafasi. Huo ni uamuzi wake siupingi, lakini nimesikitika kuona baadhi ya waliolalamikiwa wamo bado, hatuna cha kufanya zaidi ya kuwapa nafasi wafanye kazi,” alisema Zambi..

Rais Kikwete alisema kuanzia sasa Waziri atawajibika kisiasa pamoja na wote waliosababisha afikie hatua hiyo. Alisema baadhi ya viongozi wamekuwa wakilazimika kuwajibika hata kwa makosa yaliyofanywa na wengine, hivyo kuponzwa.

“Ndiyo, Waziri atawajibika kisiasa, lakini aliyesababisha Waziri awajibishwe naye hataachwa. Kama ni shirika, Ofisa Mtendaji Mkuu ataondoka na Bodi itaondoka pamoja na watendaji wakuu wa shirika au wizara,” alisema Rais.

Aliongeza kuwa katika baadhi ya maeneo, watu wamekuwa akifanya fitna ili Waziri aondoke kwa kuwajibika, wakisema walikuja wengi wakaondoka na yeye ataondoka, hivyo kuanzia sasa hilo halitakubalika.

Kuhusu ushauri wa kuigawa Wizara ya Nishati na Madini, alisema ni wazo zuri lakini alishauriwa kuwa kuunda Wizara mpya hivi sasa wakati Bajeti ilishapita ni kutafuta mzigo.

Hivyo alisema anaiacha ilivyo hadi siku zijazo kama watakaokuwapo wataona inafaa wafanye hivyo, lakini akaamua iwe na naibu mawaziri wawili mmoja ashughulike kwa kina na madini na mwingine nishati.


HABARILEO

No comments:

Post a Comment