Kufuatia Wizara ya Maji kukaa kimya bila kujibu barua toka Ofisi ya
Mbunge kwa zaidi ya mwaka mmoja, nimeamua kuchukua hatua za kibunge kwa
kuwasilisha kwa Katibu wa Bunge, taarifa na maelezo ya hoja binafsi
kutaka Bunge, katika mkutano unaotarajiwa kuanza tarehe 12 Juni 2012,
lipitishe maazimio ya kuwezesha uwajibikaji wa Wizara husika na mamlaka
zake katika kushughulikia masuala ambayo nimeyaeleza katika hoja husika.
Ikumbukwe
kwamba, tarehe 20 Mei 2012 nilitoa mwito kwa Waziri Profesa Jumanne
Maghembe kuueleza umma hatua saba za haraka zaidi za Wizara ya Maji
kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika
Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam mara baada ya Waziri kurejea
ofisini kutoka katika ziara hiyo ya vyanzo vya ruvu juu na ruvu chini na
kufanya mikutano na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) pamoja
na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO).
Nilichukua hatua
ya kutoa taarifa kwa umma baada ya Wizara kuwa na utendaji mbovu wa
kutojibu barua ambapo katika kipindi cha kati ya mwaka 2011 mpaka 2012
nimeandika jumla ya barua nne kwa Wizara husika kwa niaba ya wananchi
kwa nyakati mbalimbali bila kupata majibu yoyote.
Katika ya hatua
hizo ambazo Waziri nilieleza anapaswa kuzisimamia katika Wizara ya Maji
ni; Mosi, kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya kashfa ya taifa ya kati ya
mwaka 2003 mpaka 2010 ambapo Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na
upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na
maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation
Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika
maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji.
Pili;
kuwasilisha bungeni Mpango Maalum wa kuboresha huduma za Majisafi na
uondoaji wa Maji Taka katika Jiji la Dar es salaam uliopitishwa mwezi
Machi 2011 kwa ajili ya kuidhinishwa, kutengewa bajeti kamili ya
utekelezaji wa haraka katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kusimamiwa
ipasavyo kwa msukumo wa kibunge badala ya ahadi za ujumla za kwenye
ziara.
Tatu; Waziri kueleza hatua zilizopangwa kuchukuliwa kufuatia
ziara yake kuhakikisha Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji
ulionza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia
Juni 2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 24 uliopaswa kukamilika
Oktoba 2011 unawekewa muda wa ukomo wa kukamilika ndani ya miezi mitatu
katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa.
Nne;
Waziri kukubaliana na pendekezo nililotoa bungeni kwa nyakati mbalimbali
la Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa thamani
ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa ukarabati na
upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na
maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation
Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi (technical Audit)
uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.
Tano; Waziri
kuhakikisha Wizara ya Maji inaisimamia EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi
(performance audit) wa miradi ya visima vya maji takribani 200 ambavyo
vilichimbwa na serikali na kukabidhiwa kwa DAWASCO, jumuiya za wananchi
na taasisi mbalimbali lakini haitoi huduma inavyostahili kwa kadiri ya
malengo ya awali. Aidha, Wizara ya Maji ihakikishe EWURA inaharakisha
kutunga kanuni za udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa upande
wa sekta binafsi katika Jiji la Dar es Salaam.
Sita; Waziri
kuwezesha Kamati husika ya Bunge ijadili taarifa ya ukaguzi wa ufanisi
kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini
(performance audit report on the management of water distribution in
urban areas) ya Januari 2012 iliyotolewa na CAG kabla ya mkutano wa nane
wa bunge ulipangwa kuanza tarehe 12 Juni 2012 ili maoni na mapendekezo
yazingatiwe wakati wa mchakato wa bajeti.
Saba; Wizara ya Maji
kuhakikisha Serikali inawasilisha kwenye mkutano wa tisa wa bunge
muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali za majisafi na
majitaka (Water Supply and Sanitation Miscellaneous Amendment Bill) ili
kushughulikia upungufu uliojitokeza katika utekelezaji wa sheria
zilizopo na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.
Imetolewa Dar es salaam tarehe 8 Juni 2012 na:
John Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo

No comments:
Post a Comment