WAKATI wabunge wakitoa tuhuma nzito dhidi ya wenzao wanaodaiwa
kujihusisha na ufisadi ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),
imebainishwa kuwa wabunge wenye tabia hiyo ni watano, watatu kutoka
chama tawala CCM na wawili upinzani.
Habari
zilizopatikana jana mjini Dodoma zimeeleza kuwa baadhi ya wabunge hao
wanatoka katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, huku wengine
wakitoka Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, wabunge hao wamedaiwa kuwa wamekuwa wakitumia
nafasi zao za ubunge na ujumbe wa kamati kufanya biashara na TANESCO na
kutetea mafisadi ndani ya shirika hilo la umma.
Gazeti hili (MWANANCHI) limefanikiwa kupata majina ya wabunge hao, ambayo leo hatutayataja kwa sababu za kitaaluma.
Baadhi
ya wabunge waliochangia hoja hiyo bungeni juzi na jana walisema kuwa,
wanawafahamu wabunge hao kwa majina, lakini hawapendi kuwataja kwa kuwa
siyo wakati mwafaka.
Moto wa kutaka
kutajwa kwa majina ya wabunge hao ulikolezwa jana na Mbunge Vita Kawawa
wa Namtumbo (CCM) aliyeomba Mwongozo wa Spika, akitaka jambo hili
lijadiliwe na Bunge na kupendekeza kuwa, Kamati za Bunge zinazotuhumiwa
kwa rushwa zivunjwe, “Waheshimiwa wabunge wamejadili suala hili kwenye
wizara, lakini kwa mujibu wa kifungu cha 55 (3)f mbunge au waziri
anaweza kutoa hoja ili jambo fulani lijadiliwe. Sasa naomba kutoa hoja
ya kujadili suala hilo," Kawawa alisema.
Aliliomba
pia Bunge likubali kuivunja na kuiunda upya Kamati ya Nishati na Madini
na kamati nyingine zilizolalamikiwa kwa rushwa. Hoja hiyo iliungwa
mkono na wabunge.
Baada ya hoja hiyo
kuungwa mkono Spika wa Bunge, Anne Makinda alisimama na kukubali hoja
hiyo ya Kawawa na kutangaza kuivunja Kamati ya Nishati na Madini.
Spika
Makinda alisema ameiagiza Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge
kutengeneza kanuni za kuwadhibiti wabunge wenye tabia hiyo ya kupokea
rushwa kutoka kwa watu mbalimbali ili kutimiza matakwa yao binafsi.
"Ninakubali
kuivunja Kamati ya Nishati na Madini na zingine ambazo zitatajwa kwenye
tuhuma hizo. Nalipeleka pia suala hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili
na Madaraka ya Bunge, halafu kama ni kutajwa (wabunge hao), basi
tutapata mwongozo wa kamati hiyo." alisema Spika Makinda na kuongeza:
"Nasema kwa dhati kabisa, kitendo hiki hakikubaliki ndani ya Bunge hili.
Wabunge mkae vizuri. Kama kuna baadhi yetu wanaenda huku na huku
kujitafutia masilahi binafsi, tutawezaje kuisimamia Serikali?"
Selemani Zedi
Baada
ya Spika kutangaza kuvunja Kamati ya Nishati na Madini, Mwenyekiti wa
Kamati ya Nishati na Madini, Seleman Zedi alisema kuwa ameshtushwa na
uamuzi huo na anasubiri uamuzi wa Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya
Bunge, "Nimeshtushwa sana na uamuzi huo, lakini tusubiri Kamati ya Haki,
Kinga na Maadili ya Bunge," alisema Zedi.
Waziri Prof. Muhongo
Akihitimisha
hoja ya wizara yake bungeni jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo alisema kuwa baadhi ya wabunge ambao wanashiriki kwenye
vikao vya uamuzi vya TANESCO kama wajumbe, wamekuwa wakilihujumu
shirika hilo kwa njia mbalimbali ikiwamo kufanya nalo biashara, "Shirika
liliwahi kulipa Pauni za Uingereza 50,000 kwa ajili ya kununua vipuri,
lakini kilicholetwa nchini ni masanduku ya misumari,” alisema Profesa
Muhongo na kuongeza; “Hata katika nguzo za umeme kuna biashara
inaendelea. Tunajua kuwa nguzo hizo zinazalishwa Iringa na kupelekwa
Mombasa kisha kurudishwa nchini kwa maelezo kwamba zimetoka Afrika
Kusini."
Waziri Muhongo alisema kuwa
mbali na ufisadi huo, baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya
Nishati na Madini wamewahi kuliuzia shirika hilo matairi ya magari kwa
bei kubwa, bidhaa ambayo hata hivyo alisema haina ubora unaokubalika,
"Baadhi ya wabunge wanafanya biashara na TANESCO; niseme tu kuwa, hii
siyo sahihi. Lakini niombe kwamba mjadala huu tuufunge kwa sababu,
tayari tumekabidhi suala hilo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG)" alisema Waziri Muhongo.
Waziri
Muhongo pia alizungumzia jinsi baadhi ya watu na kampuni zinavyoiibia
TANESCO kupitia mita za Luku ambapo aliwataja watu hao kuwa ni pamoja
na Shule za St. Mary's zinazodaiwa Sh10.5 milioni, Access Bank, Tawi la
Tabata Matumbi Sh13.8 milioni na Hoteli ya Akudo Paradaise ya Kariakoo
inayodaiwa Sh25.5 milioni.
Alisema kuwa
baada ya kubainika kwa wadaiwa hao hutumia umeme kinyume na
utaratibu,wahusika wote walikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi
baada ya kufanyika kwa uchunguzi, “Baada ya kufanya uchunguzi na kubaini
kuwapo kwa watu wanaotumia umeme bila kulipia na kuisababishia TANESCO
hasara, tumeamua kuwachukulia hatua ikiwamo kuwafikisha polisi,” alisema
Profesa Muhongo na kuongeza: “Inaonyesha wazi kwamba wizi wa umeme wa
Luku umekuwa ukifanyika mara kwa mara na kwamba baada ya kuwakamata
hawa, uchunguzi utaendelea na wengine watakaobainika watachukuliwa hatua
za kisheria.”
Jenista Mhagama
Katibu
wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama alisema kuwa, amepokea kwa
masikitiko taarifa hizo za wabunge wa CCM kuingia katika tuhuma hizo,
lakini akasema namna nzuri ya kushughulikia tatizo hilo ni vyombo vya
dola kufanya uchunguzi makini ili kujiridhisha na kisha hatua za
kisheria kufuatwa, "Ni taarifa mbaya kwa kweli, lakini mimi niiombe
Serikali itusaidie kufanya uchunguzi ili ukweli ubainike na hatua
zichukuliwe," alisema Mhagama.
David Silinde
Naye
Katibu wa Wabunge wa CHADEMA, David Silinde alisema: "Kwa kuwa
tumesikia, kama kambi tutafanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo. Tutakaa
kikao cha kuamua nini cha kufanya. Pia tutatoa tamko juu ya mwenendo
mzima wa hizi tuhuma na Bunge kwa ujumla.”
Zitto Kabwe
Naye
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashirika ya Umma ambayo imeunganishwa kwenye
tuhuma hizo, Zitto Kabwe, alisema tuhuma hizo anazisikia, lakini
anaziona kama siasa za majitaka kwa sababu zinarushwa bila ushahidi
wowote, "Hakuna hata mbunge mmoja aliyesimama kusema nani amehongwa
nini. Mimi binafsi sijahongwa na mtu yeyote wala mimi sijamtetea mtu
isipokuwa natetea taratibu kufuatwa," alisema.
Zitto
alibainisha kuwa anaamini tuhuma hizo zimetokana na hasira za yeye
kupinga posho za wabunge na sasa wameona hilo ndilo eneo la kumkomoa,
"Kwa kuwa ‘my conscious is clear’, (dhamira yangu safi) sina mashaka,
uzushi, uongo na siasa za majitaka hizi zitaumbuliwa na ukweli. Hata
hivyo, kwa kuwa tuhuma hizo zinasemwa juu juu tu, tutataka vyombo vya
dola vichunguze na ikithibitika hatua zichukuliwe," alisema na kuongeza:
"Kwangu mimi naona hizi ni siasa za urais na hasira za posho. Wenye
kutaka urais wa vyama vyote na wapambe wao, wameungana kunichafulia
heshima yangu. Wabunge wenye njaa ya posho, wameungana kunikomoa. Ukweli
una tabia ya kutopenda kupuuzwa. Mwalimu Nyerere (Julius) alisema
katika andiko lake la 'Tujisahihishe'.”
Mbunge
huyo wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) alishauri pia Spika wa Bunge kutumia
Kamati ya Maadili kuchunguza tuhuma hizo kwa kuwa hazipaswi kuachwa
zikapita hivihivi.
John Cheyo
Mwenyekiti
wa Kamati ya Hesabu za Serikali, John Cheyo alisema anasikitika kuona
Bunge ambalo kimsingi ni kitovu cha uadilifu limeanza kuvamiwa na
mafisadi, "Very unfortunate, (bahati mbaya sana) Bunge ambalo ni kilele
cha uadilifu, nyumba ya waheshimiwa, ambako kunatarajiwa high level of
intergrity (uadilifu wa hali ya juu), kuanza kutumika kama perpets
(vibaraka) wa mafisadi," alisema na kuongeza: "Ninalaani sana kitendo
hicho, lakini niwaambie viongozi wapya wa Wizara ya Nishati na Madini
kuwa, waendelee kufanya kazi kwa uadilifu na nguvu yao ni wabunge wengi
wema, ambao watawaunga mkono. Wasikate tama," alisema.
Mjadala ya wabunge
John Shibuda
Mbunge
wa Maswa Magharibi (CHADEMA), John Shibuda aliliomba Bunge kufanya
uchunguzi ili kuwabaini wabunge wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Alisema
tabia ya wabunge kuendelea kusema kwa mafumbo kwamba wapo baadhi ya
wabunge wanatuhumiwa kwa rushwa, haina maana yoyote badala yake wahalifu
hao wanatakiwa watajwe hadharani.
“Mheshimiwa Spika kumekuwa na maneno hapa kwamba wapo wenzetu wanakwenda kinyume na maadili yetu.
“Hao
wanaosutwa ni bora watajwe ili wafahamike kuliko kunyamaza na kuendelea
kushutumiana kwa porojo, kwa vionjo. Bila kuwataja watu hao tutakuwa
tunalaumiana bure.
“Wabunge najisi watambuliwe. Hawa lazima watajwe kwa sababu sasa Bunge limekuwa kama bucha ya kuchinja watu, hatuwezi kukubali.
“Hivi
kuna kitu gani kilicho kama sumaku kinachowavuta wabunge mpaka waanze
kushutumiwa. Mheshimiwa Spika chunguza kwa makini uone ni sababu gani
zinazosababisha wabunge waanze kutuhumiwa katika mambo dhalimu,” alisema
Shibuda.
Aliwataka Waziri Profesa Muhongo na Katibu Mkuu, Wizara
ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi, wawe makini na ikibidi
wawachukulie hatua wafanyakazi wasiokuwa waadilifu.
“Katibu na
Waziri mmerithi makosa yasiyokuwa yenu, waondoeni wabovu kwa sababu kama
wakijiimarisha watakuwa kama vichuguu na mwishowe watajiimarisha na
kuwaharibia.
“Waondoeni makunguru maana kunguru hafugiki hata
ukimpa ubwabwa bado hafugiki. Mheshimiwa Spika tembo hubeba viroboto na
kamwe viroboto hawabebi tembo. Je, tayari mmeshawapiga risasi viroboto
wote wasiofaa?
“Waondoeni wabovu, watu najisi waondolewe kabla hawajawaondolea udhu wenu, tafadhari waondoeni hao.
“Hata
nyinyi CCM ongezeni uadilifu ili muonekane kama Serikali yenu imeokoka
na hatimaye muondokane na tingatinga linaloweza kuharibu kazi yenu,”
alisema.
Josephat Kandege Mbunge
wa Kalambo, Josephat Kandege (CCM) aliwashutumu wabunge wanaoshutumiwa
kwa rushwa ingawa hakuwataja kwa majina, “Mheshimiwa Spika ni kama siku
sita hivi wabunge wamekuwa wakijadili mambo ya baadhi ya wabunge
wenzetu. Watu hao wamekuwa wakisema hawataki posho, kumbe wana posho zao
nzito nzito ambazo walikuwa wanazitaka. Wakati wanakataa posho, sisi
tulikuwa hatuhangaiki kwa sababu tunataka hizi posho ndogo. Watu hao
wamekuwa wakijipambanua kwamba ni waaadilifu lakini Mungu akitaka
kukuumbua utaumbuka tu na nyinyi ni mashahidi. Nadhani Mheshimiwa Spika
ujumbe wangu umefika na kwa uzito niliotarajia,” alisema Kandege na
kuhamia katika mada nyingine.
Ally Keissy Mohamed
Ally
Keissy Mohamed alisema kuna haja wahalifu hao wakatajwa kwa majina kwa
kuwa hivi karibuni Profesa Muhongo na Maswi, walitumiwa ujumbe wa
vitisho kutokana na uwajibikaji wao.
Kwa mujibu wa Keissy, kama
wabunge hao hawatatajwa, viongozi hao wawili hawatakuwa na moyo wa
kufanya kazi kwa sababu baadhi ya wabunge walimfuata Maswi na kumuomba
Sh. milioni 50.
(nukuu ya gazeti la MTANZANIA)
Kangi Lgora
Naye
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora alitaka Waziri wa Nishati na Madini
awataje wabunge aliowatuhumu ili kuonyesha usawa hasa baada ya kuwataja
kwa majina watuhumiwa wengine katika ufisadi wa TANESCO na wale
wanaoliibia umeme shirika hilo la umma, "Tunaomba waziri asema kwa nini
asiwataje hao wengine wakati tayari ametutajia kina Freddy na Veronica
William Mhando na taasisi za St Mary? " alihoji.
Hoja hiyo ya Lugora ilitupwa na Spika wa Bunge Anne Makinda aliyesema kuwa jambo hilo lina taratibu zake.
Vicky Kamata
Vicky
Kimata (Viti Maalumu) nusura amwage machozi bungeni juzi jioni,
alipozungumza kwa uchungu kupinga hatua ya wabunge hao kujihusisha na
ufisadi, huku akieleza kuwa nchi imefika pabaya, 'Watanzania tumefikia
hapo! Watu wanatengeneza mgawo wa umeme ili kujipatia hela,
Jamani...jamani.. Hammwogopi hata Mungu!"
Said
Mussa Zuberi alipendekeza itungwe sheria ya kuwanyonga mafisadi na
wahujumu uchumi kwa kuwa matendo hayo pia ni uuaji, "Katika taifa letu
tuna wadudu sijui tuwaite mchwa ambao wanaharibu yaliyotengenezwa kwa
maslahi yao. Nawashauri wananchi kwa kuwa sasa tuko kwenye suala la
Katiba, wasisahau kupitisha sheria ili watu wahujumu uchumi tuwaue, tena
kwa risasi.
No comments:
Post a Comment