Makongoro Mahanga ameshinda kesi jimbo la Segerea
Dr Makongoro Mahanga
Mbunge wa Segerea, Dkt. Milton Makongoro Mahanga (CCM) amekitetea
vyema kiti chake cha Ubunge wa Segerea, Dar es Salaam kwa kushinda kesi
iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Ubunge wa jimbo hilo Fred
Mpendazoe (CHADEMA) iliyokuwa inapinga ushindi uliopatikana katika
uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010.
Mpendazoe anapaswa kulipa gharama zote za kuendesha kesi hiyo.
Hukumu
ya kesi hiyo namba 98 ya mwaka 2010 iliyosomwa leo na Jaji Profesa
Ibrahimu Juma ambaye amekuwa akiisikiliza tangu ilipofunguliwa Novemba
10, 2010, ilikuwa ikipinga ushindi wa Mahanga kwa madai kuwa sheria,
kanuni na taratibu za uchaguzi zilikiukwa katika hatua ya kuhesabu,
kujumlisha kura na kutangaza matokeo. Mbali na Dkt. Mahanga
ambaye alikuwa mdaiwa wa pili katika kesi hiyo, mdaiwa wa kwanza alikuwa
ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wa tatu alikuwa ni Msimamizi wa
Uchaguzi (RO), katika jimbo hilo.
Kutokana na dosari hizo,
Mpendazoe ambaye alikuwa akiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala,
aliiomba Mahakama itengue matokeo hayo na iamuru uitishwe uchaguzi
mwingine mdogo katika jimbo hilo au imtangaze yeye kuwa mshindi akidai
kwamba alipata jumla ya kura 56,962 na Mahanga kura 44,904. Hata hivyo,
Jaji Prof. Juma alisema ushahidi wa upande wa mlalamikaji umebainika
kuwa na mapungufu na hivyo kutupilia mbali ushahidi huo ambao uliokuwa
na hoja kumi kwa kutokukidhi matakwa ya kifungu 108 na hivyo kumpa
ushindi Dkt. Mahanga.
Dkt. Mahanga alikuwa akitetewa na Mawakili
Jerome Msemwa na Aliko Mwamanenge na AG na RO wamekuwa wakitetewa na
Mawakili wa Serikali, David Kakwaya na Seth Mkemwa.
Wakati wa
ushahidi wake, upande wa madai uliwaita mahakamani mashahidi 13 akiwemo
mlalamikaji mwenyewe Mpendazoe na wadaiwa wote watatu kwa pamoja
waliwaita jumla ya mashahidi 16.
www.wavuti.com
No comments:
Post a Comment