WALIOKUWA mawaziri katika Baraza la Mawaziri lililopanguliwa na kusukwa
upya hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete na kubaki na ubunge,
wamepangwa rasmi kwenye Kamati za Kudumu za Bunge.
Kwa mujibu wa Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliyekuwa Waziri wa
Fedha Mustafa Mkulo amepangiwa Kamati ya Maendeleo ya Jamii huku
aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja akaingizwa kwenye
Kamati ya Sheria Ndogo na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii,
Ezekiel Maige (Fedha na Uchumi).
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Cyril Chami
(Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii Dk Hadji Mponda (Katiba, Sheria na Utawala) na aliyekuwa Waziri
wa Uchukuzi Omary Nundu (Viwanda na Biashara).
Aidha, Makinda amewapangia kamati waliokuwa naibu mawaziri ambao ni
Dk Lucy Nkya aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii (Kilimo,
Mifugo na Maji) na Athuman Mfutakamba aliyekuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi
(Nishati na Madini).
Pia Spika amempangia Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Mbunge
wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) na Mbunge wa Viti
Maalumu, Subira Mgalu (CCM), amepangiwa Kamati mpya ya Fedha na Uchumi
kutoka Kamati ya awali ya LAAC.
Mgalu ameondolewa LAAC kwa kuwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza
ambapo kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge kifungu namba 113 (2),
hairuhusiwi kwa mjumbe wa kamati hiyo kuhusika moja kwa moja na
halmashauri, jambo ambalo litakuwa ni mgongano wa maslahi. Aidha,
kamati tatu za Bunge ambazo ni Fedha na Uchumi, Sheria Ndogo na Nishati
na Madini zinatarajiwa leo kuchagua wenyeviti wake wapya kutokana na
waliokuwapo awali kuteuliwa kuwa mawaziri.
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi, Dk Abdallah Kigoda
ameteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, George Simbachawene wa
Sheria Ndogo amekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na wa Nishati na
Madini, January Makamba sasa ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia.
Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia hajapangiwa kamati hadi atakapoapishwa katika Bunge.
No comments:
Post a Comment