KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda na ndugu yake,
Farijala Hussein, wamehukumiwa kifungo cha miaka 18 jela, baada ya
kukutwa na hatia katika makosa sita, yakiwemo ya kujipatia Sh bilioni
2.2 kutoka katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), iliyopo Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
Washitakiwa
wamehukumiwa kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa kwa makosa sita,
lakini adhabu hiyo inakwenda kwa pamoja kwa hivyo watatumikia miaka 3
tu.
Washitakiwa hao, walitiwa hatiani jana katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu na jopo la mahakimu watatu, Projest Kahyoza, Fatuma
Masengi na Catherine Revocath.
Mahakimu
hao, walitofautiana katika uamuzi, hali iliyosababisha kuandaa hukumu
mbili, moja iliandaliwa na mahakimu wawili, Kahyoza na Revocath na
hukumu ya pili, iliandaliwa na Masengi.
Hukumu
iliyoandikwa na mahakimu wawili ndiyo inayochukuliwa kuwa ya mahakama,
ambayo imewatia hatiani washitakiwa hao na hukumu ya Masengi iliwaachia
huru washitakiwa wote kwa madai upande wa mashitaka, ulishindwa
kuthibitisha mashitaka bila kuacha shaka.
Akisoma
hukumu ya kwanza, Kahyoza alisema washitakiwa walikuwa wanakabiliwa na
makosa saba ya kula njama, kughushi, kutoa nyaraka za uongo, kughushi,
kutoa tena nyaraka za uongo, wizi na kujipatia fedha kwa njia ya
udanganyifu.
“Katika mashitaka ya
kughushi, hakuna shaka kwamba upande wa mashitaka waliweza kuthibitisha
kosa, kwani waliokuwa wakidaiwa kuwa wamiliki halali wa Kampuni ya Money
Planner & Consultant, hawajawahi kuwepo ni wa kufikirika.
“Washitakiwa
walitumia majina hayo kwa udanganyifu, wakionyesha kwamba waliteuliwa
kuiwakilisha Kampuni ya Kijerumani, B. Grancel kudai madeni BoT wakati
si kweli,” alisema.
Alisema washitakiwa
hakuna shaka kwamba walighushi hati iliyokuwa ikiwaruhusu kuchukua
fedha za kampuni hiyo na kwamba taratibu zilifuatwa na waliwekewa kiasi
cha fedha katika akaunti yao, iliyokuwepo Benki ya Biashara Afrika.
Alisema
nyaraka za kuomba kulipwa kiasi hicho, zilikaguliwa na viongozi
mbalimbali wa BoT na kuona zilikuwa sahihi bila kubaini zimesainiwa na
upande mmoja wa Kampuni ya B. Grancel.
“Hati
zilikuwa zimesainiwa na Jonath wa Kampuni Grancel ya Ujerumani, lakini
Fundi Kitunga na Paul Thobias wa Kampuni ya Monney Planner hawakusaini.”
Upande
wa mashitaka, umeweza kuthibitisha washitakiwa walitumia hati za
kughushi kuchukua fedha BoT na shitaka la saba la kujipatia fedha kwa
njia ya udanganyifu limethibitika, kwani nyaraka za kughushi zilitumika
na shtaka hilo lilishathibitika pia.
Pia
upande wa mashitaka, uliweza kuthibitisha bila kuacha shaka kwamba,
washitakiwa walikula njama na walishindwa kuthibitisha bila kuacha shaka
katika shtaka la sita kwamba waliiba Sh 660,210,000.
Alisema
wakiachia mbali shtaka la sita, washitakiwa wanatiwa hatiani katika
mashtaka yote sita yaliyobaki kutokana na upande wa mashitaka
kuthibitisha, bila kuacha shaka kwamba walitenda makosa hayo kwa nia
mbaya.
Alisema hakuna ushahidi
uliotolewa mahakamani na upande wa mashitaka ukionyesha kwamba Kampuni
ya Kijerumani ya Gransel haikuwepo, haikuwa inaidai BoT na wala
haikuwaruhusu Kampuni ya Money Planner kudai madeni yao.
Akisoma
adhabu, Hakimu Revocath alisema washitakiwa wanahukumiwa kutumikia
kifungo cha miaka mitatu katika kila kosa kwa makosa sita, lakini adhabu
hiyo inakwenda kwa pamoja, “Washitakiwa watatumikia kifugo cha miaka
mitatu mitatu kwa kila kosa, adhabu itakwenda kwa pamoja na inaanza leo
(jana),”alisema Revocath na kuongeza adhabu hiyo kwa kosa la kwanza,
pili, tatu, nne, tano na saba.
No comments:
Post a Comment