Ni kweli kuwa katika teknolojia, zipo njia za kufanya telephone
spoofing. Zipo huduma za bure (ambazo huambatana na matangazo kila
unapotumia huduma hiyo) na ipo huduma ya kulipia ambayo haiambatani na
matangazo yoyote. Teknolojia hii si mpya duniani kwani imetumika kwa
muda mrefu sana katika nchi zilizoendelea kiasi cha baadhi ya Serikali
za nchi hizo kuzuia matumizi yake na kuweka adhabu kali kwa
atakayekutikana amekiuka sheria hizo, hii ni kutokana na teknolojia hiyo
kutumiwa kufanikisha vitendo vya kihalifu au usumbufu pasina sababu. Bofya hapa kujielimisha zaidi kuhusu "phone spoofing".
----
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimedai kugundua mbinu
zilizotumiwa na mtoto wa kigogo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) za
kuingilia mawasiliano ya simu za wabunge wake kutuma ujumbe wa vitisho
kwa mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mjumbe wa Kamati Kuu
wa CHADEMA, Mabere Marando, alisema mtoto huyo wa kigogo ambaye
hakumtaja jina, alinunua mitambo hiyo kutoka nchini Israel.
Alisema
nchini Israeli kuna kampuni mbili alizozitaja kwa majina ya Nice System
na Verinty System, ambazo zimefanikiwa kutengeneza mitambo yenye uwezo
wa kuingilia mawasiliano ya mtu kwa umbali wa kilometa tano na kwamba
moja ya mitambo hiyo ndiyo iliyotumiwa kusambaza ujumbe mfupi wa simu
kwa Mwigulu, zikionyesha kuwa zimetoka kwa wabunge wa CHADEMA.
Aliongeza
kuwa mfumo uliotumika kuingilia mawasiliano ya wabunge wa CHADEMA
unaitwa sms spoofing, na kwamba inaweza kutumiwa na idara za kiusalama
kwa sababu maalum tu.
“Tuliwauliza
wabunge wetu kama wamefanya suala hilo na wakatuhakikishia kuwa
hawahusiki, tukashtuka na kama mshauri wa masuala ya kiusalama wa chama
tukaamua kuingia kazini kufuatilia hili, tulichogundua ni kwamba mipango
hii iko nyuma ya mtoto wa kigogo wa CCM ni mtaalamu wa mitandao na ana
fedha nyingi za kufanyia kazi hii,” alisema Marando.
Alieleza
kuwa jambo la kusikitisha ni taarifa walizozipata kuwa mwanasheria mkuu
wa serikali Jaji George Werema kuwaagiza watumishi wa ofisi yake
kuandaa mashtaka kwa ajili ya tukio hilo la kuwahusisha wabunge wa
CHADEMA na meseji hizo badala ya kushughulika na watu walioingilia
mawasiliano yao.
Alisema kwa nafasi
yake, Werema kama msimamizi mkuu wa sheria nchini anajua wazi kuwa
kuingilia mawasiliano ya mtu mwingine ni kosa la jinai na mhusika
anayefanya hivyo anapaswa kushtakiwa.
“Kitendo
cha Jaji Werema kutoa maagizo ya kuandaa mashtaka kwa wabunge ni
kuwasaidia wahalifu; tunachoweza kumuambia ni kwamba taarifa tunazo
tutakutana mahakamani kuweka masuala haya wazi,” alisisitiza.
Alisema
CHADEMA haitajishughulisha kulifikisha suala hilo mahakamani bali
wanasubiri waitwe ili wakaudhihirishie umma namna viongozi wa CCM na
watendaji wengine serikalini wanavyotumia vibaya nafasi zao
kuwanyamazisha wapinzani wao kisiasa.
Alibainisha
kuwa serikali ya CCM isidhani kuwafunga mdomo wakosoaji wake wa sasa ni
suluhisho la ushindi kwao kwamba harakati za kudai uhuru wa kweli
hazikuanza sasa na hazitaishia kwa kuwadhuru watu.
Wiki
iliyopita mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu, alisimama bungeni na
kuomba mwongozo wa Spika akidai kuwa amepokea ujumbe mfupi wa simu
kutoka kwa baadhi ya wabunge wa CHADEMA, akitishiwa kuuawa.
No comments:
Post a Comment