Mshauri wa CHADEMA ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Dkt. Kitila Mkumbo, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi ya mjini Singida akikabiliwa na tuhuma za kutoa lugha ya
matusi kwa mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM).
Dkt.
Mkumbo ameunganishwa katika kesi hiyo pamoja na ofisa wa sera na
utafiti wa CHADEMA Mwita Mwikwabe (37) ambaye alisomewa pia shitaka hilo
Julai 16mwaka huu.
Awali Mwanasheria
wa serikali, Maria Mudulugu alidai kwamba Julai 14 mwaka huu, saa 10
jioni, mshtakiwa huyo alitoa lugha ya matusi kwa Mwigulu kuwa ni malaya
na mzinzi huku akijua wazi kwamba kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
Mbele
ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Ruth Masamu, mwanasheria huyo alidai kuwa
mshtakiwa alitoa lugha hiyo ya matusi kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye viwanja vya kituo cha mabasi Kijiji cha Nguvumali,
Kata ya Ndago.
Dkt. Mkumbo alikana shitaka hiko na yupo nje kwa dhamana hadi Julai 30 mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.
Nao
wakazi wawili wa Kijiji cha Nguvumali, Kata ya Ndago, Paulo Nashokigwa
(27) na Emanuel Shila (24), wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi ya mjini hapa wakikabiliwa na tuhuma za kushiriki kumuuwa
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM),
Yohana Mpinga (30).
Mwanasheria huyo
wa serikali alidai kuwa Julai 14 mwaka huu, saa 10 alasiri katika Kijiji
cha Nguvumali, Kata ya Ndago, washtakiwa wote kwa pamoja wakitumia
fimbo na mawe, walimpiga Yohana na kumsababishia kifo.
Washtakiwa
hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa vile Mahakama hiyo haina mamlaka ya
kusikiliza kesi za mauaji. Na wameunganishwa na washtakiwa wengine 12
waliosomewa shitaka lao la mauaji Julai 16 mwaka huu, kesi hiyo itatajwa
Julai 30 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment