Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbai (CHADEMA), na kada wa
chama hicho, Robert William, wamehukumiwa kifungo cha miezi saba jela au
kulipa faini ya sh 250,000 baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya
jinai.
Adhabu hiyo ilitolewa jana na
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Tabora, Thomas Simba, muda mfupi baada
ya kumwachilia huru mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho, Suzan Kiwanga,
na mwanachama mwingine, Anwaryn Kashaga.
Kasulumbai
na mwenzake walifungwa pingu na kupelekwa katika mahabusu ya mahakama
kitendo ambacho kililalamikiwa na wakili Mbogolo kwamba ni cha
udhalilishaji na uvunjaji wa haki za binadamu.
“Unakifurahia
kitendo unachokifanya? Alisikika Kasulumbai akimuuliza askari polisi
aliyemvika pingu mara baada ya hukumu hiyo kutolewa.
Akisoma
hukumu ya kesi hiyo, hakimu Simba alisema kuwa hii ni sawa na kesi
nyingine zinazowakabili watu wengine kwamba mbunge huyo atakwenda jela
miezi mitatu kwa kutoa lugha ya matusi au kulipa faini ya sh 50,000.
Pia
aliwahukumu washtakiwa hao kwenda jela miezi minne au kulipa faini ya
sh 100,000 baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la shambulio liletalo
madhara mwilini.
Hakimu Simba vile vile
aliwataka washtakiwa hao kumlipa fidia ya sh 2,000,000 mlalamikaji
Fatuma Kimario, ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga.
Washtakiwa wote walilipa faini hiyo na kuachiliwa huru huku wakibaki kusubiri kulipa fidia hiyo ya sh milioni moja kila mmoja.
Awali
upande wa mashtaka ulidai kuwa washtakiwa wote walitenda makosa hayo
Septamba 15 mwaka jana, katika Kijiji cha Isakamaliwa wilaya ya Igunga.
Mara
baada ya kuachiliwa huru, Kiwanga na Kashaga walitoka nje na kutimua
mbio jambo lililowafanya watu waliokuwepo mahakamani hapo kuwashangaa.
Mapema
wakili wa utetezi, Edson Mbogolo, aliiomba mahakama itoe adhabu ndogo
kwa wateja wake kwa vile ni wakosaji wa mara ya kwanza na kwamba
Kasulumbai (62) ana watoto 27 na wake watatu wanaomtegemea.
“Mahakama
izingatie kwamba Kasulumbai ni mwakilishi wa wananchi na endapo akipewa
adhabu ya kifungo, jimbo lake litakuwa wazi na hivyo litaigharimu
serikali kuitisha upya uchaguzi,” alisema Mbogolo.
Makosa
mengine yaliyokuwa yakiwakabili washtakiwa hao ni kumweka chini ya
ulinzi isivyo halali kwa mujibu wa sheria Mkuu huyo wa Wilaya, huku kosa
la nne ni wizi kutoka maungoni ambalo halikuweza kuthibitishwa na hivyo
kufutwa na mahakama.
No comments:
Post a Comment