Na mwandishi wetu
Musoma,
WATOTO watatu wa familia moja wamewafikisha wazazi wao katika kituo
kikuu cha Polisi Mjini Musoma kitengo cha dawati la jinsia na watoto
wakidai kutelekezwa na kuwafanya kuishi maisha ya kutangatanga mitaani
ili hali wazazi wao wakiwepo na kuendelea na maisha ya kila siku bila
kujua wao wanaishi vipi.
Wakiongea nje ya kituo hicho cha Polisi, mmoja wa watoto hao
aliyejitambulisha kwa jina la Justine Kichere amesema baba yao mzazi kwa
kushirikiana na mama yao wa kambo ambaye hawakuweza kumtaja jina lake
waliwafukuza nyumbani kwa kuwatupia nguo zao kwa kile walichokieleza
kudaiwa kuwa (machokoraa) watoto wa mitaani.
Wakielezea chanzo cha tukio hilo la kufukuzwa nyumbani,Justine mwenye
umri wa miaka 14 mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi
Rwamlimi A iliyopo Manispaa ya Musoma amesema waliitwa na mama yao wa
kambo akiwa na wadogo zake wawili James Kichere mwenye umri wa miaka 13
na Gerald kichere mwenye umri wa miaka 12 na kuelezwa kuwa mama yao
anaumwa na amelazwa katika hospitali ya Mkoa hivyo kuwataka kwenda
kumsalimia mama yao.
Mtoto huyo alieleza kuwa wakiwa njiani kuelekea hospitalini huku
wakiwa hawapajui waliomba msaada katika gari moja nakueleza wanakwenda
katika hospitali ya Mkoa na kupandishwa kisha kuelekea wasipokujua na
walipofika na kuuliza waliambiwa wapo maeneo ya Ramadi.
Alidai baada ya kudaiwa kupotea waliomba msaada wa kurudi nyumbani
Musoma na kusaidiwa lakini mara baada ya kufika nyumbani bila kuulizwa
kilichowasibu walitupiwa nguo zao nje na kutakiwa kuondoka nyumbani na
watafute mahala pengine watakapo kwenda kuishi.
Justine amesema baada ya kufukuzwa na baba yao pamoja na mama yao wa
kambo waliamua kwenda kwa mama yao ambaye alitengana na baba yao
anayeishi maeneo ya Baruti na kukaa kwa muda wa siku mbili kisha mama
yao kuwataka kurudi kwa baba yao kwa kuwaeleza kuwa hana pesa ya
kuwalisha wote watatu.
Aliendelea kueleza baada ya kuona hawana sehemu ya kwenda waliamua
kutaka kuingia katika maisha ya mtaanii na waliishi katika maisha hayo
kwa muda wa wiki moja huku wakiwa wakilala katika jumba bovu maeneo ya
Nyakato na kuyaona maisha hayo hawayawezi na kuamua kwenda kituo cha
Polisi ili kuweza kupata msaada zaidi.
Mtoto huyo aliongeza kuwa hilo sio tukio la kwanza kwa baba yao
Kichere Sangi aliyemueleza kuwa ni mfanyabiashara wa duka la rejareja
katika maeneo ya Kigera kufanya hivyo kwa kuwa alishawahi kumfukuza kaka
yao Geofrey Kichere aliyekuwa akisoma kidato cha tatu katika shule ya
sekondari Bweri ambaye mpaka sasa hajulikani halipo.
Aidha watoto hao wamesema lengo la kwenda katika kituo cha Polisi ni
kutaka kupata msaada kwa kuwa maisha wanayoishi mtaani ni magumu na
wameshindwa kwenda shuleni huku mmoja wao akiwa anakabiliwa na mtihani
wa darasa la saba
BINDA NEWS Ilifika katika ofisi ya dawati la jinsia na watoto katika
kituo cha Polisi Musoma kutaka kujua hatima ya watoto hao na kuelezwa
kuwa wanazotaarifa hizo na hatua waliyochukua ni kundika barua wa wito
kwa wazazi ili kuelezea madai ya watoto hao.
Short URL: http://www.thehabari.com

No comments:
Post a Comment